Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kimbe: Siasa zinaiua Mbeya City

Mbeya City Kushuka Wachezaji wa Mbeya City

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

“Mbeya City iwe kampuni”. Ni jambo analolisisitiza aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe ambaye alitangaza kuachia nafasi hiyo hivi karibuni, huku akisema siasa zinachangia kuikwamisha timu hiyo kurudi Ligi Kuu.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika jijini hapa, Kimbe aliyedumu madarakani kwa muda mrefu, kwa sasa amesema amepumzika uongozi ila kwenye mpira yupo sana.

Kiongozi huyo aliiongoza Mbeya City kwa miaka 12 akianza nayo ngazi za chini tangu kusajiliwa kwake 2011 hadi Novemba 2023 alipotangaza kuachana na timu hiyo akibaki kuwa mdau tu.

Kimbe mwenye misimamo yake, amefunguka mengi ikiwamo kilichoishusha daraja City, tamu na chungu zilizomkuta kipindi cha uongozi wake.

MALENGO YALITIMIA?

Anasema malengo yake yalitimia kwa kiasi fulani japokuwa mengine hakuyafikia, akieleza kuwa anajivunia kuipandisha timu Ligi Kuu, kuiweka kwenye ushindani na kuipa nembo iliyowabamba mashabiki.

Pia anasema City ilikuwa miongoni mwa timu zilizodumu kwa muda mrefu Ligi Kuu kwani tangu ilipopanda haikushuka kwa miaka 10 mfululizo suala ambalo kwake ni mafanikio.

Anaeleza kuwa licha ya mafanikio hayo, lakini yapo mambo mawili ambayo hakuyafikia ikiwa ni kutokamilika kwa mchakato wa timu kuwa mfumo wa kampuni akieleza kuwa atakayerithi nafasi yake ajitahidi kulitimiza.

Anasema alikwama kufikia lengo hilo kutokana na ugumu wa kupatikana kwa fedha ambazo zilihitajika kutokana na mfumo wa kiutawala, japokuwa kama timu isingeshuka daraja alikuwa katika mazungumzo ya mwisho na taasisi moja ya kifedha.

“Baada ya kuanza mchakato tulikuwa na mfululizo wa vikao ambapo kila siku tukikutana tunaanza upya, pesa za kuanzia zikakosekana hadi tukakwama kufikia lengo japokuwa 2018 tulisajili kampuni, ishu ikawa pesa za uendeshaji.

“Ila baadaye kuna benki moja ilionyesha nia kutaka kuwekeza na tulikuwa hatua za mwisho ndio timu ikashuka daraja na mipango ikaishia hapo hivyo ili City iwe bora lazima mfumo wa kampuni ukamilike na siyo kusubiri bajeti ya Jiji.

Kigogo huyo anaongeza kuwa jambo jingine ni kutokamilisha mpango wa kuandaa makocha wawili kuwa na leseni A ya Caf akieleza hata hivyo amewaandaa wataalamu wengi.

“Kwa miaka 12 ninajivunia wachezaji wengi nilioibua, makocha kama Mohamed Kijuso, Juma Mwambusi, Maka Mwalwisi na wengine.

“Na hadi sasa nilikuwa kwenye mpango wa kuwasomesha makocha wawili kupata leseni A ya Caf lakini naona mkakati huo haujatimia, nilipenda sana falsafa iliyopo Ulaya kwa kuwapa nafasi wachezaji wao,” anasema Kimbe.

TUHUMA NA LAWAMA

Mara kadhaa mashabiki wa Mbeya City walikuwa wakimtuhumu kigogo huyo kwa kashfa mbalimbali ikiwamo upigaji kwenye timu wakisema bajeti inayowekwa haitumiki vilivyo.

Hata hivyo, kauli za mashabiki hao zilikuwa zikija kipindi ambacho timu inapambana na matokeo yasiyoridhisha wakienda mbali zaidi kumtaka aachie ngazi.

“Tuhuma nilizisikia lakini nilipuuzia nikajua wanaozungumza hawajui kitu, kama pesa ilikuwa inaidhinishwa na Halmashauri kama ningeweza kuzipiga ningebaki hadi leo?

“Na sikukata tamaa kwa sababu Mbeya City inao mashabiki wa aina nne, wapo wasiopenda mpira, wasiopenda Simba na Yanga na wale wakereketwa wa Simba na Yanga.”

Anasema alikuwa katika wakati mgumu pale City ilipokuwa ikizifunga Simba na Yanga, hali ambayo ilimuweka kwenye migogoro hadi na baadhi ya viongozi wa Jiji.

“Mtu ni kiongozi lakini anakwambia umeifunga timu yangu hivyo hata ijayo ushinde lakini nilihakikisha nafanya kazi yangu japokuwa maneno yalikuja kutokana na kuzifunga hizo timu.”

Anaongeza kuwa hata viongozi wa timu hizo kongwe nchini wamekuwa wakitofautiana naye kutokana na misimamo yake akihakikisha timu inacheza na aliyejiandaa ashinde uwanjani.

“Ni tukio moja tu ambalo lilinisononesha walipotuhumu kwamba tumeuza mchezo dhidi ya Azam FC wakati wakitwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila ya kupoteza mchezo wowote msimu ule wa 2012-2013, ule mchezo tulifungwa (2-1) kihalali hakukuwapo na ishu yoyote,” anasema Kimbe.

KILICHOISHUSHA MBEYA CITY

Kiongozi huyo bila kufafanua zaidi, anasema timu hiyo ilihujumiwa na baadhi ya wadau akisema hawezi kuwataja lakini ni walewale wa karibu kwa hila zao.

Pia anazitaja siasa kuchangia kwa kiasi fulani akieleza kuwa timu hiyo inamilikiwa na Halmashauri na wenye maamuzi ni madiwani ambao wanaunganishwa na siasa.

“Tulihujumiwa tu na watu wa karibu wala hawakutoka mbali, lakini hata siasa nazo zimechangia kwa sababu ile ni timu ya Halmashauri ambayo inaongozwa na wanasiasa.”

Anaongeza kuwa changamoto nyingine ni uwekezaji kwani Halmashauri ina mambo mengi ya kufanya na mpira siyo kipaumbele, ndio maana anasisitiza timu iwe kampuni.

“Na kama hawajui timu ilikuwa chanzo cha mapato kwa sababu tulikuwa na udhamini wa ligi na binafsi, viingilio getini yote hiyo imepotea, watapaswa kutafuta chanzo kingine.”

Anabainisha kuwa timu haiwezi kuendeshwa kwa michango ya mashabiki akizitolea mifano baadhi ya timu zilizotegemea nguvu ya mashabiki na kupoteana hadi leo.

KUIKAMIA SIMBA

City ikiwa Ligi Kuu ilikuwa mwiba mkali kwa timu kongwe nchini hususani Simba hadi kuwaibua mashabiki wakidai inaikamia timu moja wakieleza kuwa huenda ikawa sababu ya kushuka kwake.

Kimbe anakanusha vikali akieleza kuwa Simba haikuwa inakamiwa kwenye Ligi Kuu tu, bali ni timu ambayo hata mechi za kirafiki Mbeya City ikiwa Daraja la Kwanza hawakushinda.

“Hata Yanga nao tumewasumbua sana hapa Sokoine japokuwa tukiwa Dar es Salaam ndio wametufunga sana, Simba hata mechi za kirafiki hawakutufunga ila mashabiki kila mmoja anazungumza tu.”

Kimbe anashauri kuwa bado uwezekano wa timu hiyo kurudi Ligi Kuu upo, iwapo wataweka mkakati wa uwekezaji na kuisuka timu vizuri na pia kusimamia mchakato wa kuwa kampuni.

NGUVU YA MASHABIKI

Wakati Mbeya City ikipanda Ligi Kuu msimu wa 2012/13 ilikuwa na mzuka mwingi wa mashabiki waliokuwa wakisafiri na timu hiyo popote na pia sapoti yao ilikuwa si ya mchezo.

Hata hivyo, kadri siku zilivyosogea, nguvu yao ni kama ilipotea, ambapo Kimbe anafafanua kuwa uongozi ulikuwa ukiwawezesha kila kitu, lakini waliiweka timu karibu yao.

Anasema kuwa kipindi hicho timu iliweka kambi katika Chuo cha Kilimo Uyole ambako ilikuwa ni kituo cha wanafunzi na mashabiki wengi kuifikia hata wakati wa mechi waliweza kuwasiliana.

“Uongozi ulijitahidi kutafuta usafiri lakini kambi ikawa kule Chuo cha Kilimo Uyole, ikifika muda wa mechi wanapeana taarifa wanapanda magari kwa shangwe wanakuja uwanjani,” anasema Kimbe.

KUHUSU UUZAJI VIFAA

Mbeya City ni kati ya timu zilizopanda Ligi Kuu kwa mapinduzi makubwa ikiwamo uuzaji vifaa klabuni ikiwamo jezi na skafu, ambapo baadaye ilipotea na kuacha maswali.

Anafichua kuwa waliamua kuachana na biashara hiyo kufuatia hujuma nyingi walizobaini kwa watengenezaji wenyewe.

“Tuligundua biashara hii ni haramu, kwani hata watengenezaji wanashiriki njama hizi kuhujumu vifaa tukaamua kuachana nayo, hata ukipata kampuni za nje gharama yake ni kubwa kulinganisha na uwezo wa mashabiki.”

ILIPOTOKA

Kimbe anasema wazo la kupata timu lilianza 2009 wakati wa michuano ya serikali za mitaa (Shimisemita), ambapo Jiji lilikuwa chini ya Mkurugenzi Juma Idd aliyekuwa mtu aliyependa michezo.

Anasema pamoja na ushiriki wao wa michuano hiyo walikuwa wakihitaji kitu cha kuwaunganisha haswa wale ambao hawana mlengo wa kisiasa ili waweze kukutana huko.

“Rasmi timu ilisajiliwa 2011 tukanunua timu ya Rhino iliyokuwa Daraja la Kwanza Arusha na msimu wa kwanza hatukupanda, hadi wa pili tulipofanikiwa nikiwa katibu mkuu.

“Tulikuwa na matokeo mazuri kwa msimu wa kwanza kumaliza nafasi ya tatu, msimu wa pili nafasi ya nne na hii ilitokana na mipango ya uongozi kwani hakukuwapo mgogoro wowote.”

Anaongeza kuwa wakati wanapanda Ligi Kuu bajeti yao ilikuwa Sh6 milioni kwa mshahara wa wachezaji kila mwezi na Sh16 milioni kwa usajili.

“Kimsingi wachezaji walijituma bila kuwa na majina makubwa wakapambana kutafuta maisha timu ikawa ndani ya nafasi tatu za juu kwa mara ya kwanza Ligi Kuu kisha nafasi ya nne.

“Mafanikio hayo ilitokana na kujituma kwa wachezaji, hatukuwa na mgogoro wowote kiuongozi lakini kuhusu hatma yangu nimepumzika kwa sasa uongozi ila lolote linaweza kutokea popote watakaponihitaji,” anasema Kimbe.

Chanzo: Mwanaspoti