Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kimataifa uswapimie shughuli yao

Simba Kimataifa Simba wakishangilia goli dhidi ya RS Berkane

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba ya kimataifa ni habari nyingine. Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, jana waliupiga mwingi na kubakisha pointi tatu nyingine nyumbani baada ya kuichapa RS Berkane kwa bao 1-0 katika mchezo uliojaa vurugu.

Ushindi wa jana ni wa pili kwa Simba ikiwa nyumbani awali ikiinyoa Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyokuwa uwanjani usiku wa jana kuvaana na US Gendermarie ya Niger katika kundi hilo, na kuifanya sasa ifikishe alama saba baada ya mechi nne.

Aidha, ushindi huo ulilipa kisasi cha kipigo cha 2-0 ilichopewa ugenini wiki iliyopita umeiweka Simba pazuri katika msimamo katika kupenya hatua ya robo fainali.

Katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na ulioruhusiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuhudhuriwa mashabiki 35,000, wageni walionekana kulalamikia uamuzi ya refa Jean-Jacques Ngambo Ndala kutokana na baadhi ya matukio ya uamuzi wa kutatanisha uwanjani.

Pape Ousmane Sakho aliyeng’ara kwenye mchezo huo, alifunga bao tamu kwa kuwachambua mabeki watatu wa Berkane, bao lililolalamikiwa na wageni, kwani Meddie Kagere alikuwa katika eneo la kuotea mara mbili ndani ya sekunde chache kabla ya kufungwa kwa bao hilo. Awali aliupokea mpira akitokea katika eneo la kuotea akamrudishia mfungaji na wakati Sakho akipiga shuti la bao, Kagere aliendelea kuwa mbele ya kipa na akauruka mpira akiwa katika eneo la kuotea.

Malalamiko yao hayakuwaokoa, na siku yao mbaya ilihitimishwa kwa mwamuzi kutowapa penalti waliyoidai baada ya mshambuliaji wao kugongana na kipa Aishi Manula na pia kukataliwa kwa bao walilodhani wamefunga lakini mwamuzi msaidizi aliinua kibendera cha kuashiria mfungaji aliotea.

Simba walikaribia kupata bao la pili, lakini shuti la mtokea-benchini, Bernard Morrison liligonga besela kwenye kona ya juu anakotagia ndege huku kipa wa Berkane akiwa ameshakubali yaishe.

Kiujumla mechi ilijaa matukio ya msuguano na mwamuzi Ndala huku mara kadhaa watu wa benchi la Berkane wakivamia uwanjani kupinga uamuzi wa refa huyo kutoka DRC.

Kiungo wa Simba Sadio Kanoute alimchezea vibaya Adama Ba, tukio lilisababisha vuta nikuvute kati ya wachezaji wa pande zote Berkane wakilalamikia kitu alichofanya Kanoute, aliyelimwa kadi ya njano sambamba na Sofian Moudane aliyeonekana kufokeana na mwamuzi huyo.

Winga wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda alitiwa mfukoni na hakuwa na madhara hadi akatolewa.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji Simba ikiwatoa Kibu aliyerejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu na kumuingia Bernard Morrison aliyeongeza kasi ya mashambulizi.

Wengine walioingia ni Chris Mugalu, Mzamiru Yassin, Taddeo Lwanga na Peter Banda kuwapokea, Jonas Mkude, Bwalya, Kagere na Sakho, huku Berkane nao wakiwatoa Kisinda, BA aliyepata maumivu na Fekkak nafasi zao zikichukuliwa na Elmehdi Oubilla, Mohammed Farehane, Brahim Bahraoui.

Simba: Manula, Kapombe, Tshabalala, Onyango, Inonga, Mkude/Lwanga, Kibu/Morrison, Kanoute, Kagere/Mugalu, Bwalya/amiru, Sakho/Banda

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz