Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kim tuoneshe utofauti Stars

Ab939684a9476b28b39b9879237e474d Kim tuoneshe utofauti Stars

Sat, 13 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MIAKA ya hivi karibuni Tanzania imeonesha jitihada kwenye soka katika kufuzu michuano ya Afrika.

Imeshiriki Chan, U17, U20 na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘Afcon’. Kufika hatua hiyo kwa kweli ni mafanikio makubwa na hatua muhimu katika maendeleo ya soka.

Lakini pamoja na jitihada hizo bado Tanzania haijaonesha ubora pale inapofuzu na kwenda kushindana kwenye mashindano hayo, kwani timu zote hizo hakuna iliyoonesha matumaini angalau kuvuka hatua moja kwenda nyingine.

Timu zimekuwa zikiishia hatua ya makundi na hapo ndipo mwisho wa ubora kitu, ambacho kinajenga taswira na mtizamo mbaya kwa mashabiki wa soka kuwa Tanzania hamna kitu.

Pale wanapoona wachezaji kadhaa wameteuliwa au kocha fulani ndio amepewa kukinoa kikosi fulani, basi utaona maneno pale hamna kitu tutatolewa mapema.

Kwanini wanasema hivyo? uchunguzi mdogo unaonesha wazi kuwa hawana imani na waliopewa majukumu kwa maana makocha au kikosi kilichoteuliwa kuwakilisha kulingana na ukubwa wa mashindano.

Hawana imani kwasababu wanawajua namna walivyo wababaishaji baadhi yao uzuri wameshafundisha katika baadhi ya timu za Ligi Kuu na ukichunguza utagundua hakuna mafanikio kokote walikopita.

Hao ni makocha, hata wachezaji wanaoteuliwa, wanaopangwa, namna wanavyocheza kuanzia mechi za kirafiki inadhihirisha uwezo wao.

Waliovurunda huko nyuma wameshatimuliwa, sasa macho ya Watanzania wanamtizama Kocha aliyekabidhiwa jukumu jipya kwa maana ya Kim Poulsen.

Kocha huyo kutoka Denmark ana kazi ya kuhakikisha Stars inafuzu fainali za Afrika na kibarua chake cha kwanza atacheza dhidi ya Guinea ya Ikweta Machi 22, mwaka huu ugenini kisha atarudi nyumbani kucheza mchezo mwingine dhidi ya Libya mwishoni mwa mwezi huu.

Poulsen sio mgeni sana hapa nchini aliwahi kufundisha huko nyuma kuanzia timu za vijana na hata Stars kwa hiyo anawajua wachezaji wengi hasa wale wakongwe hivyo, hatopata kazi sana.

Watanzania wanataka kuona utofauti wake anakuja na nini kipya? mfumo wake utakuwaje mbali na wale waliopita? Na kikosi chake cha kwanza ni kipi? je, atapanga kikosi cha majaribio kama baadhi ya waliopita au atawapanga wale wazoefu.

Kazi ni kubwa kwake na wengi wana imani naye kuwa anaweza kufanya vizuri ikiwa tu kuna jambo jipya amewaletea Watanzania.

Kitu cha kwanza ni kuhakikisha Stars inafuzu Afcon kisha wanakwenda kushindana bila kujali ni nani na ana ukubwa gani kwasababu soka limebadilika hakuna tena ule mfumo wa kuogopa majina makubwa.

Namna watakavyocheza na timu hizo za kiushindani itajenga picha nzuri tunakoelekea. Kwasababu mechi hizo hazitakuwa rahisi kila mmoja anapambana kivyake kutafuta nafasi ya kufuzu.

Wachezaji pia, wanaopewa nafasi na Kocha huyo waoneshe thamani yao kwanini wamechaguliwa.

Wanatakiwa wajitoe kwa ajili ya taifa kwa kucheza soka la kuvutia kutomwangusha Kocha ambaye amewaamini na kuwaita akiwategemea watafanya kile anochowaelekeza.

Kocha ana kikosi chake kabla ya kucheza michezo ya kufuzu atakutana na Harambee Stars ya Kenya kujipima nao nguvu. Pia, mchezo huo ni kipimo kizuri na hapo taratibu uwezo wake utaanza kuonekana.

Ingawa ni changamoto kwake hasa ikizingatiwa amepewa timu ni kipindi kifupi cha maandalizi kuelekea michezo hiyo ya kufuzu.

Pengine kama angepata timu tofauti za kucheza michezo ya kujipima angekuwa amejua nani anastahili kuanza nan ani anaanzia benchi. Kingine, ni kwamba baadhi ya wachezaji wanatumikia klabu zao michuano ya kimataifa watachelewa kujiunga nao ili kutengeneza muunganiko wake mapema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz