Kwenye mfumo wa kisasa, mchezo wa soka unatajwa kuendana zaidi na wachezaji vijana. Soka la kisasa linahitaji nguvu na kasi uwanjani, ndio maana inaelezwa kuwa huo ni mchezo unaowahusu vijana zaidi kwani wao bado wana uwezo wa kutenda hayo kwa ufanisi zaidi.
Lakini kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajia kitamatika Juni 9 kuna wachezaji ambao wanatajwa kuwa umri umeanza kuwatupa mkono, hata hivyo bado wanatamba na kucheza kwa viwango vikubwa na kushindana na vijana.
Mfano mzuri wa wachezaji hao ni Kelvin Yondani, ambaye pamoja na kuwa na umri mkubwa, lakini jambo hilo halionekani kuwa kikwazo kwake.
Wakati ligi hiyo ikielekea ukingoni na Yanga kutawazwa Mabingwa, Mwanaspoti linakuletea kikosi cha wakongwe ambao wanaendekea kukiwasha.
Mastaa hawa wamekuwa chachu ya ushindani ndani ya soka la Tanzania bara wakicheza sambamba na vijana huku wachezaji wengine walio na umri Mdogo wakiwekwa benchi kuwapisha wakongwe hao wacheze.
DEOGRATIUS MUNISHI (NAMUNGO)
Ndiye kipa aliyecheza muda mrefu zaidi miongoni mwa makipa waliopo katika vikosi mbalimbali vya timu za Ligi Kuu baada ya Juma Kaseja, Ally Mustafa ‘Bartez’ kustaafu na kuamua kuingia kwenye ukocha. Dida amecheza kwa mafanikio makubwa ligi kuu akipata nafasi ya kucheza timu zote kubwa Simba, Yanga na Azam FC sasa anakipiga Namungo aliyojiunga akitokea Mbeya city.
HARUNA SHAMTE (GEITA GOLD)
Beki huyo wa kulia aliyewahi kutamba na Toto Africans, Simba, Mbeya City, JKT Tanzania, Lipuli na sasa Geita Gold ni moja ya walinzi hodali ambao wanaendelea kutoa changamoto kwa damu changa na kuongeza ubora wa ligi.
Shamte licha ya kudumu kwenye soka muda mrefu bado anaendelea kutoa changamoto kwenye kikosi cha Geita Gold huku akiwasumbua washambuliaji wa timu pinzani.
DAVID LUHENDE (KAGERA SUGAR)
Mkongwe aliyedumu kwa muda ndani ya kikosi cha Kagera Sugar alianza Mwadui FC, Yanga na alishawahi kukupiga Mtibwa Sugar ni beki ambaye pamoja na ukongwe wake anaheshima yake awapo kwenye majukumu.
Beki huyo wa kushoto wa Kagera Sugar ni kati ya mabeki wenye sura za kazi wawapo uwanjani. Huyu haogopi kunyakua mpira miguu mwa washambuliaji hata akiwa ndani ya eneo la 18.
Sio muoga wa kupambana wala kuhofia kupata kadi kwa namna anavyocheza kwa mabavu dhidi ya wapinzani wake, na ni findi wa kupiga pasi za mwisho pamoja na ukongwe wake ameendeleza ubora ambao ulimfanya kocha wa timu ya taifa kumjumuisha kwenye kikosi chake hivi karibuni.
PASCAL WAWA (SINGIDA BS)
Ni moja ya wachezaji wa kigeni ambao wanatajwa kwa mafanikio kwenye soka la Tanzania alianza kuitumikia Azam FC na baadae akajiunga na Simba ambayo ameichezea kwa mafanikio makubwa akitwana mataji matatu na kucheza robo fainali mbili Ligi ya Mabigwa na Kombe la Shirikisho Afrika moja.
Wawa amekuwa na muendelezo mzuri ndani ya kikosi hicho kutokana na kufanikiwa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza na amekuwa akionyesha ubora wake katika eneo la ulinzi, Namna anavyookoa mipira ya hatari golini kwao kwa mshambuliaji muoga hawezi kulisogelea hovyo lango.
JUMA NYOSSO (IHEFU FC)
Ukiachana na matukio yake ya utovu wa nidhamu ambayo alikuwa anafungiwa fungiwa na TFF, Nyosso anapokuwa uwanjani ana sura ya kazi kiasi kwamba hakuna straika anayekwenda kizembe eneo lake pamoja na ukongwe wake ameendelea kuwa msaada kwenye kila timu anayopata nafasi ya kuichezea.
Nyoso sio beki anayeogopa kuwavaa kimabavu washambuliaji wa timu upinzani, na kubwa zaidi analoliangalia ni kuondoa mpira kwenye eneo la hatari la mlinda mlango wake hiyo ndio Siri yake ya mafanikio ambayo inamfanya aendelee kuwa imara na tishio kwa washambuliaji.
ERASTO NYONI (SIMBA)
Huu ni mwake wake wa 18 dimbani tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2005 katika kikosi cha AFC Arusha. Nyoni aliwahi kucheza soka ya kulipwa Vital O ya Burundi kabla ya kutua Azam.
Kwa sasa ni mchezaji wa Simba na Taifa Stars, akiwa ndiye mchezaji mkongwe zaidi, lakini ubora wake umempa nafasi ya kuwemo katika kikosi cha kwanza cha Simba akiwaacha vijana wanasota benchi.
AMISSI TAMBWE (SINGIDA BIG STARS)
Ni Mshambuliaji mwenye rekodi yake kwenye soka la Tanzania amecheza timu zote kubwa kwa mafanikio akifumania nyavu kwa nyakati tofauti huku pande zote mbili Simba na Yanga akiibuka mfungaji bora.
Pamoja na kutemwa na Yanga hakutaka kurudi kwao kwani alijiunga na timu ya daraja la chini Championship ambapo pia aliendeleza makali yake akiibuka mfungaji bora baada ya kupachika mabao 14 na kuisaidia Singida Big Stars kupanda daraja sasa hana msimu mzuri akiwa ndani ya timu hiyo.
RAMADHANI CHOMBO (POLISI TZ)
Amejiunga na Polisi Tanzania akitokea Geita Gold ambayo aliipa mafanikio kwa kuisaidia kushiriki mashindano ya kimataifa msimu uliopita baada ya kumaliza nafasi ya tatu na kupata fulsa ya kushiriko Kombe la Shirikisho Afrika ambapo pia walifanikiwa kufanya vizuri ukata ukiwakwamisha.
Redondo miguu wake ndani ya Polisi Tanzania haujawa mzuri kutokana na timu hiyo kushuka daraja, kiungo huyo fundi alisajiliwa Ashanti United mwaka 2008 akitokea Norway ambako alikaa miaka minne, huko alipelekwa na kituo cha soka cha kukuza vipaji kwa vijana kiitwacho Dar Youth Olympic Centre (Dyoc), kilichopo Chang’ombe TCC, jijini Dar es Salaam.
Ulipofika usajili wa dirisha dogo mwaka 2010, Simba walivutiwa na mchezaji huyo na kuanza kusaka saini yake na walifanikiwa kumnasa ingawa aliichezea timu hiyo kwa msimu mmoja kisha kutimkia Azam FC, mwaka 2012/2013 na msimu uliofuata anarudi tena Simba akapotea kwa muda akar udi Geita Gold sasa Polisi Tanzania.
MEDDIE KAGERE (SINGIDA BS)
Amejiunga na SBS akitokea Simba hajaonyesha makali yake kama alivyofanya akiwa msimbazi baada ya kutwaa kiatu cha dhahabu mara mbili mfululizo akianza msimu wa 2018/19 mabao 23, 2019/20 mabao 22. Kwa sasa hana makali sana ndani ya timu yake ambaye ameichezea kwa misimu miwili sasa na hajafanikiwa kutwaa kiatu hata mara moja.
JACOB MASSAWE (NAMUNGO)
Ni mkongwe ambaye anaendekea kutarna Ligi Kuu ya Bara kama kiungo, kisha beki na sasa straika, Jacob Massawe ‘Le Captain’, ni moja ya wachezaji waliocheza timu zaidi ya tatu kacheza Stand United, Ndanda FC, Gwambina na sasa Namungo.
Mkongwe huyo ambaye amecheza nafasi nyingi uwanjani kwa mafanikio anaendekea kukiwasha akiwa Namungo FC na ni mchezaji ambaye anacheza kikosi cha kwanza tangu amejiunga na timu hiyo.
SAIDO NTIBAZONKIZA (SIMBA)
Ni mchezaji anayeongoza kwa pasi za mwisho akitoa 12 hadi sasa na anamfukuzia Fiston Mayele kwenye kinyang’anyiro cha ufungaji bora wa msimu huu baada ya kupachika mabao 15 akiachwa nyuma bao moja tu na Mayele mwenye 16 (hii ni kabla ya mechi za jana za kufungia msimu.)
Ntibazonkiza amecheza timu mbili msimu huu akianzia Geita Gold ambayo ameichezea nusu msimu na kujiunga na Simba ambayo amemalizia miezi sita ili kutimiza mwaka mmoja.
KOCHA HANS PLUIJM (SINGIDA BS)
Huyu ndiye kocha mkongwe ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu akiwa na uzoefu mkubwa wa kuwahi kuzifundisha Yanga, Singida United na Azam kabla ya kutua Singida Bis Stars, inayoshiriki ligi kwa msimu wake wa kwanza na kufanikiwa kukata tiketi ya CAF kwa kumaliza katika Nne Bora.
Mbali na kumaliza ndani ya Nne Biora sambamba na Yanga, Simba na Azam, pia timu hiyo ni kati ya nne zilizofika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) iking'olewa na Yanga ambayo itaumana na Azam kwenye mechi itakayopigwa keshokutwa Jumatatu, jijini Tanga.