Kocha wa timu ya Taifa ya DR Congo, Sebastien Desabre, amesema kupoteza nafasi za kufunga mabao ndiyo sababu iliyofanya timu yake ishindwe kufika fainali ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2023).
Michuano ya Afcon inaendelea nchini Ivory Coast kwa sasa ikiwa hatua ya fainali na mshindi wa tatu, baada ya Afrika Kusini na Congo kuchapwa kwenye michezo ya nusu fainali, juzi.
Congo ya beki wa Simba, Henock Inonga, ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Ivory Coast kwenye mchezo uliokuwa mkali na wa kuvutia kwa dakika zote tisini.
Ivory Coast ambayo ilianza vibaya michuano hii baada ya kushinda nechi moja tu hatua ya makundi, ilijipatia bao kupitia kwa mshambuliaji wake mahiri Sebastien Haller.
“Jambo la kwanza kwangu ni masikitiko kuhusu mchezo huu, tulipata nafasi nyingi sana lakini tukashindwa kuzitumia na hilo ndiyo jambo lililotunyima kwenda fainali.
“Hatukutumia vyema nafasi ambazo tulitengeneza, nilibadili aina ya kucheza, tukafanya na mabadiliko ya baadhi ya wachezaji, lakini hatukupata kile ambacho tulikuwa tunategemea, lazima hili lituumize.
“Lakini tunawaachia watu watambue kuwa kulikuwa na timu bora kwenye michuano ya Afcon mwaka huu, tunaumia kwa kuwa hatukufanya vizuri na kufika fainali, lakini tunatakiwa kuhakikisha tunasahau haya kwa kuwa bado tuna mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, lazima tuungane ili tumalize michuano hii tukiwa washindi.”