JKT Tanzania waliingia na 'game plan' nzuri ya kuhakikisha wanawazuia Yanga wasiweze kugongeana zile pasi za haraka hususan katika dimba la kati hata hivyo, walibana kisha wakaachia goli 5-0, kilichowaponza kimebainishwa.
Mchambuzi mmoja ambaye alikuwa akifuatilia mtanange huo uliopigwa jana Agosti 29, 2023 katika Uwanja wa Azam Comlex jijini Dar alisema, JKT walizidiwa kwenye uwezo (quality) wa mchezaji mmojammoja wa Yanga.
"Angalia JKT walivyokuwa wanacheza, walikuwa wakifanya makosa mengi sana lakini walau kwa kipindi cha kwanza safu yao ya kiungo na ulinzi ilikuwa makini kidogo kuweza kuharibu mipango ya Yanga lakini uwezo mkubwa wa Aziz Ki uliweza kuwatanguliza Yanga kwa goli moja ikiwa ni dakika ya mwisho ya mchezo ya kipindi cha kwanza," alisema mchambuzi huyo.
Mchambuzi huyo alisema, Aziz Ki ndiye aliyefungua koki ya magoli kwani kipindi cha pili, JKT walirudi na mkakati wa kushambulia kutafuta nafasi ya kusawazisha badala ya kubaki kwenye mpango wao na kujikuta wakitoa nafasi kwa Yanga kuweza kucheza kwenye eneo lao na kupata magoli zaidi.
"Kipindi cha pili JKT walitoka kabisa kwenye game plan yao na kujikuta wakiwapa nafasi zaidi Yanga ya kushambulia kukiwa na nafasi nyingi za wazi na bahati mbaya JKT walionekana kuchoka na kufanya makosa mengi katika kipindi cha pili, wakaadhibiwa," alisema mchambuzi huyo.
Yanga waliongeza goli la pili kupitia kwa Kennedy Musonda ambaye alipokea pasi kutoka kwa Nickson Kibabage kisha Yao Kwasi akatupia la tatu na mwisho Max Nzengeli akaweka misumali miwili ya mwisho mtawalia.