Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichomwondoa Maxime Kagera Sugar ni hiki

Mecky Maxime Best Coach Kilichomwondoa Maxime Kagera Sugar ni hiki

Sun, 24 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Juzi Kagera Sugar ilitangaza kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime kwa makubaliano yao ya pande mbili ikiwa ni siku moja tu baada ya kikosi hicho kupoteza mabao 4-0, dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ililiambia Mwanaspoti sababu kubwa ya Maxime kupewa mkono wa kwaheri ni kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya wachezaji jambo ambalo ndio chanzo cha kufanya vibaya.

“Alipoteza trust (uaminifu) kwa wachezaji na baadhi wakapeleka malalamiko yao kwa viongozi wa juu wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kabla ya mambo hayajaharibika, ndipo ukafanyika uchunguzi wa kina na kugundua hilo,” kilisema chanzo hicho.

Mtoa taarifa huyo alieleza bado walikuwa na imani kubwa na kocha huyo kutokana na mchango wake alioutoa katika timu hiyo ingawa wameamua kufanya uamuzi huo mgumu kwa mustakabali wa kikosi hicho ambacho kimekuwa hakina matokeo mazuri.

Kwa upande wa Maxime akizungumzia hilo alisema makubaliano yaliyofanyika ni ya pande mbili hivyo alisema hawezi kuzungumzia zaidi kwa sasa.

Maxime alirudi Kagera Sugar Oktoba 30, mwaka jana kuchukua nafasi ya Mkenya, Francis Baraza aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabovu na ameiongoza katika michezo 13 ya Ligi Kuu Bara, akishinda mitatu, sare minne na kupoteza sita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live