Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichomuua Suleiman Mathew hiki hapa!

Afarikiiiiii Kilichomuua Suleiman Mathew hiki hapa!

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Saa chache baada ya kutolewa kwa taarifa kwamba nyota wa zamani wa Tukuyu Stars, Simba na Yanga, Suleiman Mathew amefariki dunia asubuhi hii, chanzo kilichomuua staa huyo aliyemudu beki ya kati kimeanikwa hadharani.

Mathew alikumbwa na umauti akiwa amelazwa katika hospitali ya Amana (sio Temeke kama ilivyoelezwa mwanzoni) baada ya kuanza kuugua mara aliporudi kutoka Kanda ya Ziwa ikielezwa alikunywa supu iliyomletea matatizo ya tumbo hadi akafanyiwa upasuaji wa tumbo.

Mwanaspoti limezungumza na mastaa mbalimbali waliowahi kucheza na nyota huyo na wengine wakiwa ni watu wake wa karibu waliokuwa wanamtembelea akiwa amelazwa Amana kwamba walipata muda wa kuzungumza naye, ndio waliofichua chanzo cha tatizo lililomsababishia kufanyiwa upasuaji wa utumbo.

Staa wa zamani wa Simba, Madatta Lubigisa amesimulia jinsi alivyoambiwa na marehemu Mathew; "Alikuwa safari ya kikazi huko Kanda ya Ziwa, aliniambia amekunywa supu, lakini anaona tumbo linamuuma, akasafirishwa hadi hospitali ya Amana.

"Baada ya kufika Amana, akafanyiwa upasuaji, lakini ilipofika Alhamisi alianza kujisikia vibaya akawa anatapika njano, hadi tukawa tunajadiliana naye ili afanyiwe uchunguzi zaidi," amesema Madatta na kuongeza;

"Kwangu alikuwa baba, mtu wa karibu sana, pamoja na kwamba alikuwa hospitalini bado alikuwa ananituma kufuatilia baadhi ya vitu, kwani ndiye alikuwa anasimamia kuanzishwa kwa ligi ya malegendari na huko Kanda ya Ziwa alikuwa anaandikisha watu wa kushiriki na inatarajiwa ianze mwezi ujao, itakuwa inachezwa kama Ligi Kuu kwa maana ya nyumbani na ugenini."

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Idd Moshi amesema; "Mathew amefariki alfajiri ya leo Jumapili katika hospitali ya Amana, alifanyiwa upasuaji wa utumbo, kuhusu ratiba ya mazishi itawekwa wazi, bado ndugu hawajakaa wapo katika hali ya mshituko na msiba upo kwake Vijibweni, Kigamboni."

Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba na Yanga, Shaaban Ramadhan amesema; "Wakati tunamtembelea hospitalini Amana, hakuwa anaonyesha hali ya mahututi, ambayo ingetupa ishara ya kifo chake, ila mapema aliniambia alikunywa supu akiwa Kanda ya Ziwa na kuanza kusumbuliwa na tumbo, hadi mauti yalipomfika."

Enzi za uhai wake, Mathew alikuwa mmoja wa wachezaji waliotwaa ubingwa wa Ligi ya Bara akiwa na Tukuyu Stars, kisha kuzichezea Simba, Yanga na Ndovu ya Arusha mbali na kusimamia wachezaji na baadaye kuingia kwenye siasa akichaguliwa katika uchaguzi mdogo kuwa Diwani wa Vijibweni kupitia CCM mwaka 2012 na mwaka 2015 akagombea Ubunge Jimbo la Mtama, Lindi linaloshikiliwa na Waziri Nape Nnauye, kupitia Chadema kabla ya mwaka 2021 kutangaza kurejea CCM.

Chanzo: Mwanaspoti