Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichomuondoa Kocha Sven-Goran Eriksson

Skynews Sven Goran Eriksson 6662267 Meneja wa zamani wa timu ya Taifa ya England Sven-Goran Eriksson

Tue, 27 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya England, Sven-Goran Eriksson amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76 baada ya kusumbuliwa na saratani ya kongosho.

Kocha, Eriksson, ambaye alikinoa kikosi cha England maarufu kama Three Lions kwa miaka mitano, aliiongoza timu hiyo kufika hatua ya robo fainali mara mbili kwenye fainali za Kombe la Dunia na michuano ya Euro.

Eriksson, ambaye alikuwa kocha kwenye kikosi cha England kilichodaiwa kuwa ni kizazi cha dhahabu, alifichua Januari mwaka huu kwamba alikuwa na kipindi kisichozidi mwaka mmoja cha kuwa hai baada ya kugundulika kuwa na saratani.

Na jana, Jumatatu familia yake ilithibitisha kocha huyo kufariki dunia.

Taarifa ya familia hiyo ilisomeka hivi: “Sven-Goran Eriksson amefariki dunia. Baada ya kuugua kwa muda mrefu, SGE alifariki dunia asubuhi nyumbani kwake akiwa amezungukwa na familia yake.”

Familia hiyo ilihitaji suala hilo liachwe kwa familia ili kuomboleza kwa utulivu msiba huo.

Eriksson, ambaye ni raia wa Sweden, alikuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa timu ya soka ya taifa ya wanaume ya England mwaka 2001, ambapo kwenye kikosi chake kulikuwa na mastaa wa maana kama David Beckham, Steven Gerrard, Wayne Rooney na Frank Lampard.

Eriksson aling’atuka kuinoa England baada ya fainali za Kombe la Dunia 2006 na baadaye alikwenda kufanya kazi kwenye soka la timu za klabu na timu nyingine za taifa. Kutokana na matatizo yake ya kiafya alilazimika kung’atuka kwenye nafasi yake ya kuwa mkurugenzi wa michezo kwenye klabu ya Karlstad ya Sweden, Februari 2023. Baada ya kutangaza kuwa na saratani, Eriksson alifichua ndoto ya maisha yake wakati alipowaongoza magwiji wa Liverpool katika mechi ya hisani dhidi ya Ajax iliyofanyika Anfield, Machi mwaka huu.

Eriksson alipofichua maradhi yake alisema: “Kila mtu afahamu kwamba nina maradhi ambayo si mazuri kabisa. Kila mtu anafahamu ni saratani. Lakini nimepambana nayo kwa kadri ninavyoweza.”

Baada ya hapo, Eriksson alifichua kwamba hana muda unaozidi mwaka mmoja wa kuendelea kuwa hai, lakini pia anaweza kuwa na muda zaidi.

Kocha huyo aliwaambia wachezaji wake, wasihuzunike, bali watabasamu tu. Baadhi ya mastaa ambao amewanoa kocha huyo ni pamoja na Lampard, Gerrard, Rio Ferdinand, Paul Scholes, Beckham na Michael Owen.

Kikosi chake cha England kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006 kilikomea kwenye hatua ya robo fainali. Baada ya kuachia ngazi, alikwenda kuinoa Manchester City kwa mwaka mmoja kisha akarudi tena kwenye soka la kimataifa alipoinoa Mexico na Ivory Coast.

Baada ya kuinoa Leicester City, kocha huyo alikwenda kufanya kazi kwa miaka minne Chinese Super League.

Kazi yake ya mwisho kwenye ukocha, Eriksson alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Philippines hadi mwaka 2019 na hapo alipohitimisha pazia lake la ukocha. Kocha huyo mkongwe, alizaliwa Februari 5, 1948. Na kipindi chake alipokuwa mchezaji, alikuwa beki wa kulia katika klabu ya Torsby.

Alistaafu soka kama mchezaji alipokuwa na umri wa miaka 27, alienda kuwa msaidizi huko Degerfors na baadaye akawa kocha mkuu mwaka 1977.

Mwaka huo huo, Eriksson alioa mke wake wa kwanza, mrembo Ann-Christine Pettersson, ambaye walizaa watoto wawili.

Chanzo: Mwanaspoti