Dar es Salaam. KIUNGO wa Yanga, Mukoko Tonombe ‘Ticha’ juzi alianza kwa mara ya kwanza kikosi cha kwanza cha timu hiyo katika Ligi Kuu ya msimu huu, halafu akafunga bao la tatu akimalizia pasi tamu ya Farid Mussa na kushuhudiwa akimwaga chozi wakati wa kuishangilia bao hilo na wenzake.
Mukoko aliyeanza kwenye nafasi ya Khalid Aucho, alifunga bao hilo dakika 75 likiwa la kwanza kwake msimu huu, lakini lililoihakikishia Yanga kuzoa alama tatu mbele ya Ruvu Shooting walioinyuka mabao 3-1 na mwenyewe amefunguka kilichomliza kwenye Kwa Mkapa.
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mchezo huo, Mukoko alisema alilia kwa kushindwa kujizuia kutokana na mengi ambayo yalikuwa nyuma yake kabla ya mchezo huo.
Mukoko alisema kabla ya mchezo kupata nafasi ilikuwa ngumu kwake kwani kuna wakati alitakiwa asiwepo katika wachezaji 20, watakavaa jezi kwenye mechi hiyo hata wale wa kikosi cha kwanza.
Alisema baada ya kupata nafasi ya kuwepo katika kikosi cha kwanza alijiapiza na kujiwekea malengo anataka kucheza kwa kiwango cha juu mno ili kuisaidia timu kupata ushindi.
“Nimekuwa nikipitia wakati mgumu, msimu uliopita baada ya kupata kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Simba mambo yamekuwa sio mazuri kwa maisha yangu ya soka,” alisema Mukoko na kuongeza;
“Kuna wakati nilijikuta nakata tamaa na kulia nikiwa peke yangu kambini na nyumbani ndio maana baada ya kufunga nilijikuta nalia kwa furaha iliyochanganyikana na uchungu. Niwashukuru mashabiki wote wa Yanga walioonyesha kuwa nami katika kipindi chote kigumu. Nawaahidi kuwapa raha zaidi.”
Alisema bao hilo alililofunga amelitoa kama zawadi kwa mashabiki wote wa Yanga wanaoendelea kumuamini licha ya kuwepo ushindani wa namba katika kikosi chao kwa sasa.
Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi alisema Mukoko alikuwa nje katika baadhi ya mechi kutokana na adhabu yake huku wachezaji waliocheza kwenye nafasi hiyo walifanya vyema.
“Ilikuwa ngumu kuwaondoa haraka ndio maana nimeanza kumpa nafasi katika kikosi taratibu akitokea benchi na katika mechi ya ruvu alifanya vizuri, lakini haikuwa ngumu kucheza kutokana na Khalid Aucho kuumia nyonga,” alisema Nabi.
Kuhusu Saido Nabi alisema alikuwa akimweka nje Saido Ntibazonkiza kutokana na masuala ya kinidhamu lakini si kama hakuwa katika kiwango bora.
Nabi alisema baada ya kutambua kosa lake alimfuata na kumuomba nae kama kocha, mzazi na mlezi wa timu aliamua kumsamehe na kumpa tena nafasi kikosini.