Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichombakisha Aziz KI Yanga ni hiki

Aziz Ki Yangaaa Mobetto Kilichombakisha Aziz KI Yanga ni hiki

Thu, 11 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Habari ikufikie Mwananchi ya kwamba, kiungo mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki ataendelea kuwa ndani ya kikosi cha Young Africans SC kwa misimu miwili ijayo.

Hiyo ni baada ya kuongeza mkataba wa miaka miwili baada ya ule wa awali kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita 2023-2024.

Aziz Ki ambaye alijiunga na Young Africans SC msimu wa 2022-2023 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ameitumikia timu hiyo kwa misimu miwili, hivyo kuongeza miaka miwili mingine inamaanisha kwamba ni mali ya Wananchi kwa miaka minne.

Ndani ya misimu hiyo miwili ya kwanza, Aziz Ki amekuwa na mchango mkubwa wa upatikanaji wa mafanikio ikiwemo makombe ya Ligi Kuu ya NBC na FA ambayo yote wamebeba misimu mawili mfululizo yeye akiwemo Ngao ya Jamii mara moja.

Aziz Ki pia anakumbukwa kwa namna ambavyo msimu wa 2022-2023 ambao yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, goli lake pekee katika mchezo wa marudiano dhidi ya Club Africain tukiwa ugenini, ndilo liliipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya michuano hiyo na kuwa safari ya kwenda fainali ikachochewa hapo.

Msimu uliopita ambao ilibaki kidogo tufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Aziz Ki alifunga goli ambalo lilikataliwa dhidi ya Mamelodi Sundowns ugenini.

Goli hilo lilizua mjadala mkubwa katika soka la Afrika na nje ya bara hili huku baadaye Rais wa CAF, Patrice Motsepe akikiri wazi kwamba lilikuwa goli halali ingawa maamuzi ya VAR ililikataa kwa madai mpira haukuvuka mstari.

Aziz Ki katika misimu miwili ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na jezi ya Young Africans, amefanikiwa kufunga jumla ya magoli 30 na hat trick tatu.

Msimu wa 2022-2023 alifunga magoli 9 ikiwemo hat trick moja dhidi ya Kagera Sugar, huku msimu wa 2023-2024 akifunga magoli 21 na hat trick mbili dhidi ya Azam na Tanzania Prisons kisha akaibuka kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.

Aziz Ki ameonekana kuvutiwa na project ya Young Africans kutaka kubeba ubingwa wa Afrika na usajili mzuri uliofanyika kitu kilichompa matumaini makubwa ya kufikia malengo yake ndiyo maana ameamua kuongeza mkataba huo.

Ikumbukwe kwamba, nyota huyo raia wa Burkina Faso, alikuwa akiwindwa vikali na timu kubwa barani Afrika ikiwemo Mamelodi Sundowns, CR Belouzidad, Wydad Casablanca, Al Ahly, Raja Casablanca na nyinginezo, lakini akaamua kubaki Young Africans.

Aziz Ki hakubaki tu kirahisi, bali ushawishi mkubwa alionao mwekezaji wa klabu hiyo, Gharib Said Mohamed (GSM) na Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said umesababisha yote hayo kutokea.

Injinia Hersi ndiye aliyemshawishi mara ya kwanza kusaini Young Africans kipindi anatoka ASEC Mimosas kwani nyota huyo pia alikuwa akiwindwa na timu kubwa za ndani ya Afrika na Ulaya, lakini ushawishi huo unaochagizwa na GSM na project iliyopo ikamvutia Kiungo huyo.

Kuongeza mkataba kwa Aziz Ki ni sehemu ya kuendelea kuboresha kikosi cha Wananchi kuelekea msimu ujao ambapo hadi sasa tumewaongezea mikataba wachezaji saba waliokuwa na timu msimu uliopita.

Wachezaji hao ni Aboutwalib Mshery, Djigui Diarra, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Farid Mussa na Aziz Ki.

Mbali na hao, kuna maingizo mapya ya wachezaji watano ambao ni Clatous Chama, Prince Dube, Chadrack Boka, Khumeiny Aboubakar na Aziz Andambwile.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live