Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichojificha nyuma ya pazia 'Supu Day' ya Wananchi Jangwani

Supuuuu A0016 Kilichojificha nyuma ya pazia 'Supu Day' ya Wananchi Jangwani

Sat, 2 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Supu yake chapati mbili. Ndio msemo uliozoeleka, ila pale Jangwani, wenyewe waliibuka na chapati 500 kwa mashabiki wakati wanakunywa supu wiki mbili zilizopita. Yanga ilikuwa ikisherehekea ushindi wa mabao 5-1 iliyopita mbele ya Simba.

Ilikuwa ni tukio flani amaizingi katika maisha ya soka. Utamu zaidi unaambiwa hadi mashabiki wa Simba nao walijichanganya kuichangamkia supu hiyo ilitokana na ng’ombe watano iliyopewa klabu hiyo kwa ushindi huo.

Juzi kati tena wakapelekewa ng’ombe watano kutoka Paul Makonda ikiwa ni shangwe hizo hizo, mabosi wa Yanga wakaamua kuwagawa kwa mashabiki na wahitaji wengine. Kifupi ni kwamba kuna maisha flani hivi ya akili nyingi Yanga inayaishi ikijitofautisha na klabu nyingine nchini kwa mambo mawili wanayoyafanya kwa msimu wa tatu sasa.

Kubwa lililovutia ni kuwaandalia mashabiki na wanachama supu safii na kila mmoja akapata bakuli lake na chapati za kutosha.

Inaelezwa supu hiyo imesaidia kuwafanya wanachama na mashabiki kujiona wana thamani mbali na kuwekwa karibu klabuni.

Sasa kama hujui ni kwamba Yanga imekuwa ikifanya shughuli flani za kijamii sambamba na kufikika kirahisi kwa wanachama na mashabiki kupitia mambo mbalimbali wanayoyafanya kwa watu wao.

Kuna mambo mengi wanayofanywa ila baadhi ambayo ndani yake yanakwenda kupanda kitu kizito ndani ya  mioyo ya watu hao na kwa mambo haya kama yanamkuta mtu ambaye anayumba kwa imani ya klabu hiyo ni rahisi kumsomba na kujikuta anaingia ndani ya klabu hiyo bila ya kupenda. KILA MECHI WANATOA

Kama umewafuatilia Yanga kila sehemu wanayoenda kucheza mechi, basi kuna jambo wanalifanya siku moja kabla au mapema siku ya mchezo husika ikiwamo kutoa msaada kwenye kituo cha yatima au watu wenye uhitaji.

Hiki wanafanya katika kila mchezo ambao wanacheza ndani ya nchi, lakini kama haitoshi hata wakienda nje ya nchi wamekuwa wakifanya vivyo hivyo.

Lilifanyika kule DR Congo walipoenda kucheza na TP Mazembe msimu uliopita na wakajizolea mashabiki wengi na kama haitoshi walipokwenda Rwanda na Algeria hivi karibuni walifanya tena kitu cha namna hiyo na watu wa kule wakajikuta wanashangazwa na kitu cha namna hiyo.

Mbaya zaidi hata kama wakipoteza, huwa hawajali bado wamekuwa wakiendelea kutoa misaada ya namna hiyo wakishiriana na wafadhili wa klabu hiyo yaani Kampuni ya GSM.

MASHABIKI NA MASTAA Wakiwa kwenye shughuli hizo za kijamii Yanga wangeweza kwenda viongozi pekee kufanya kazi hiyo, lakini wao wamekuwa wakienda mbali zaidi kwa kuwachukua makocha na hata wachezaji kufika katika kazi hizo, hili limekuwa linawafanya mashabiki na wanachama wao kuona ni jinsi gani nao wako karibu na kikosi chao.

Ukiacha kuwaona wachezaji wao viwanjani, lakini mashabiki wamekuwa wakijikuta wako pembeni ya kina Stephanie Aziz KI, Djigui Diarra, Miguel Gamondi na kupanda imani kubwa zaidi ya klabu hiyo.

SUPU KWA MASHABIKI Baada Yanga kuichapa Simba kwa mabao 5-1 kusherehekea ushindi huo wakafanya tukio moja pale klabuni kwao kwa kuchinja ng’ombe, kisha kutengeneza supu kwa mashabiki na wanachama wao na watu kujaa wengi wakaburudika na chakula hicho wakiwemo pia mashabiki baadhi wa klabu nyingine kama Simba waliojichana.

KUFUNGUA MATAWI Yanga pia imekuwa ikifanya kazi ya kufungua matawi kokote wanakokwenda, matawi hayo ndio fedha kwa klabu na hili limekuwa likianza tangu utawala wa Dk Mshindo Msolla, lakini hata aliyemfuata Injinia Hersi Said naye ameendeleza hilo kwa kuwa hapo kabla walikuwa wakishirikiana naye kuyafanya hayo.

Hivi juzi tumeona hilo linaendelea wakifungua tawi moja la watu waioona tukio ambalo liliwagusa wengi kw namna ambavyo Hersi na wasaidizi wake kufika kwa mashabiki hao na  kuwapa mualiko wa kuja uwanjani kuangalia mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

WAGONJWA WAMO Wamekuwa pia wakikumbuka wenye maradhi mbalimbali katika shughuli hizo, ebu kumbuka yule kijana mdogo Ally Kimara anayesumbuliwa na changamoto ya upumuaji kwamiaka zaidi ya nane,  alivyofanyiwa sapraizi na Yanga akiwa hawezi kufanya lolote, lakini anaishangilia timu hiyo akiwa kitandani ni namna gani aliguswa kwa matukio yale mawili ya kumfuata nyumbani na hata kuletwa uwanjani Yumo pia daktari mmoja ambaye anaugua maradhi kama hayo Yanga ilimfuata nyumbani na hata kumleta uwanjani jinsi gani alifarijika kwa tukio lile la kuwa karibu na klabu anayoipenda.

SIKU MAALUM KWA MASTAA Msimu huu, Yanga ikaja na mpya zaidi ya kutambulisha matukio flani ya mechi kwa  kubebwa na kugeuzwa siku maalum za wachezaji wao kwa jinsi wanavyoonekana, kuvaa na hata mahala wanakotoka.

Kazi hiyo ikaanza kwa Maxi Nzengeli ambaye ni maarufu kwa kuchomekea jezi kisha akafuata Stephanie Aziz KI anayependa kukunja bukta yake na mashabiki kuvaa vipensi.

Sasa imekuja na Siku ya Ibrahim Hamad ‘Bacca’  ikiitwa Bacca Day’ kwa ajili ya mechi ya kesho ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly,  hii ikizidi kuwasogeza mashabiki wao na wanachama karibu na klabu yao kwa kuifuatilia na hata kuvuna watu wapya kwa kuwa matukio haya yote yana mvuto kwa jamii.

WACHEZAJI WANABADILIKA Viongozi na wafadhili wa Yanga wanapofanya hivi mastaa wao nao wanaonekana kuanza kuambukizwa matukio hayo, kwani  wameanza kufanya mambo kwa jamii wanazotoka waanzilishi wakiwa ni mabeki na nahodha Bakar Mwamnyeto na kiungo Zawadi Mauya, waliokuwa na siku maalum kwa ajili ya taasisi zao Wamo pia Dickson Job na Kibwana Shomari, pia walikuja na siku maalum za kutoa misaada kwa jamii kwa kufanya hisani ikisindikizwa na mechi maalum.

Matukio kama haya yanafanya klabu kuheshimika, pia kuonyesha uungwana kwa watu wanaowazunguka kitu ambacho ni vyema kikaigwa na klabu nyingine katika kuimarisha mshikamano kwa jamii wanazozishabikia.

NINI MAANA YAKE? Akizungumzia hilo Mtendaji Mkuu wa zamani wa Yanga, ambaye kwa sasa ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ya Botswana, Senzo Mazingisa anasema hatua iliyopigwa na Yanga kwa kufanya shughuli hizi za kijamii na kuwafuata wanachama ni moja ya mafanikio makubwa yatakayowapa faida kwenye maeneo mbalimbali kiuchumi.

Senzo aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba kabla ya kuhamia Yanga anasema kwa shughuli hizo klabu hiyo haitumii nguvu kubwa kugeuza furaha ya wadau hao kuchangamkia fursa za mauzo ya jezi, mashabiki kujaa viwanjani pia imekuwa ikizinufaisha klabu nyingine.

“Wakati hili linaanza nilikuwapo Yanga tulijua matunda yake yatakuwa makubwa, leo kama ukienda kwenye mfumo sahihi wa taarifa Yanga itakuwa na idadi kubwa ya watu,” anasema Senzo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live