Dar es Salaam. Muunganiko mzuri wa safu ya kiungo jana uliifanya Yanga kucheza soka maridadi na kupata mabao matatu dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nidhamu ya safu ya kiungo iliyokuwa ikichezwa na Feisal Salum na Rafael Daudi iliwapa wakati mgumu wachezaji wa JKT Tanzania kudhibiti pasi zilizokuwa zikipenyezwa kwa washambuliaji wa Yanga.
Nahodha wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto alikuwa na kazi ngumu kuwadhibiti akina Feisal waliokuwa wakibadilika mara kwa mara kulingana na kasi ya mchezo.
Wakati Feisal alikuwa na kazi moja ya kudhibiti kasi ya Kazimoto, Daudi alikuwa na fursa nzuri ya kutawala eneo la kiungo hatua iliyompa nafasi ya kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji wa Yanga.
Yanga iliendelea kudhibiti eneo la kiungo hata alipoingia Thabani Kamusoko kujaza nafasi ya Daudi aliyetoka kipindi cha pili moto ulikuwa ni uleule.
Kasi ya washambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo, Mrisho Ngassa na Ibrahim Ajibu, iliwavuruga mabeki wa JKT Tanzania.
Wachezaji hao kila mmoja alifunga bao na kuchangia ushindi wa mabao 3-0 iliyopata Yanga katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga imefikisha pointi 35 ikiiteremsha kileleni Azam kwa kuipiku pointi mbili ingawa zinalingana kwa idadi ya mechi 13 ilizocheza kila moja. Simba imezidiwa pointi nane na Yanga ikiwa nafasi ya tatu.
Makambo aliyefunga bao la kwanza dakika ya 19 amefikisha mabao saba nyuma ya kinara wa mabao Eliud Ambokile wa Mbeya City mwenye manane.
Licha ya Yanga kupata ushindi, JKT Tanzania ilicheza kwa nidhamu kwa kuwa muda mrefu wa mchezo ilifanya mashambulizi mara kwa mara langoni mwa Yanga na kama siyo uhodari wa kipa Ramadhani Kabwili, timu hiyo ingepata zaidi ya mabao mawili.
Yanga ilipata bao la pili katika dakika 52 lililofungwa na Ngassa.
Ajibu alifunga bao la tatu dakika ya 72 kwa penalti baada ya beki wa JKT Tanzania kushika mpira ndani ya eneo la hatari.
Abdulrahman Mussa wa JKT Tanzania alikosa mabao licha ya kupata nafasi nzuri dakika ya 23 na 34 ambapo mashuti yake hafifu yalidakwa na Kabwili.
Katika hali isiyotarajiwa, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema wachezaji wake walicheza bila kula kutokana na mabadiliko ya ratiba.
Ratiba ya awali, ilionyesha mchezo huo ulipangwa kuchezwa saa 12:00 jioni kabla ya kupigwa saa 10:00. “Nawapongeza wachezaji wangu ndani ya siku nane wamecheza mechi tatu tukiwa tunasafiri kwenye viwanja tofauti,” alisema Zahera.
Yanga: Ramadhani Kabwili, Paul Godfrey, Haji Mwinyi, Abdallah Shaibu, Andrew Vincent, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Cleofas Sospeter, Raphael Daud/Thabani Kamusoko, Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu na Deus Kaseke.