Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila vita ishafungwa La Liga 2023-24

Madrid X Betiss Kila vita ishafungwa La Liga 2023-24

Sat, 25 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Pazia la mikikimikiki ya La Liga kwa msimu wa 2023-24 litafungwa rasmi wikiendi hii, ambapo mechi moja ilifanyika usiku wa jana, wakati Girona ilipokuwa nyumbani kukipiga na Granada.

Mechi kibao zitapigwa leo Jumamosi, ambapo Osasuna itakuwa mwenyeji wa Villarreal, wakati Real Sociedad itakipiga na Atletico Madrid, wakati Almeria itamaliza ubishi na Cadiz, Rayo Vallecano itacheza na Athletic Bilbao, huku Real Madrid itajimwaga uwanjani Bernabeu kucheza na Real Betis.

Mchakamchaka wa ligi hiyo utaendelea kesho Jumapili, ambapo Getafe itakuwa na shughuli pevu mbele ya Mallorca, wakati Celta Vigo itaonyeshana kazi na Valencia, La Palmas itaonyeshana kazi na Deportivo Alaves huku mchezo wa mwisho utashuhudia Sevilla ikikipiga na Barcelona.

Kwenye La Liga msimu huu, ishu ya ubingwa imeshamaliza muda mrefu baada ya Real Madrid kukamatia taji hilo, huku itaingia uwanjani kwenye mchezo wao wa mwisho kuweka heshima tu, ikisaka nafasi ya kufikisha pointi 97, lakini pia ikitafuta rekodi ya kushinda mechi 30 kwenye ligi.

Kwenye mechi 37 ilizocheza Los Blancos hadi sasa, imeshinda 29, sare saba na upoteza moja tu, huku ikiwa imefunga mabao 87 na kufungwa 26 pekee.

Mahasimu wao Barcelona kwa msimu huu, mambo hayakuwa mazuri sana, ikijihakikishia nafasi ya pili hata kama itapoteza kwenye mchezo wao wa mwisho watakaokabiliana na Sevilla ugenini.

Barca imevuna pointi 82 katika mechi 37 ilizocheza, ikiwa imeshinda 25, sare saba na kupoteza tano, imefunga mabao 77 na kufungwa 43.

Wapinzani wao kwenye kusaka nafasi ya pili, Girona imetibua dakika za mwisho na hivyo itamaliza kwenye nafasi ya tatu hata kama itakuwa imeshinda mchezo wao wa usiku wa jana Ijumaa. Hata hivyo, nafasi hiyo imewapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikimaliza nafasi ya juu kuliko wababe, Atletico Madrid, ambao safari hii imeishia kwenye nafasi ya nne, baada ya kukusanya pointi 73 katika mechi 37 ilizocheza.

Kwenye msimamo wa La Liga, nafasi tano za juu, ambazo zinatoa tiketi za kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, zimeshajipanga na hakutakuwa na mabadiliko yoyote katika kuelekea mechi za mwisho wa msimu. Timu nyingine zenye nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, Real Sociedad kwenye nafasi ya sita na Real Betis kwenye namba saba.

Hata hivyo, kwenye La Liga, vita nyingi zitamalizwa mapema, kwani hadi timu tatu zitakazoshuka daraja zimeshafahamika, ambapo Almeria imeungana na timu za Granada na Cadiz, ambazo hazitakuwapo kwenye ligi hiyo msimu wa 2024-25.

Almeria imemaliza msimu kwenye nafasi ya mwisho kabisa kwenye msimamo, ikivuna pointi 18 katika mechi 37, ikiwa imeshinda mbili, sare 12 na vichapo 23. Granada ilikuwa na shughuli usiku wa jana kwa kumenyana na Girona, kabla ya mechi hiyo ya mwisho kwao, ilikuwa imeshinda nne tu kwenye mechi 37 na kuvuna pointi 21.

Katika mechi 37, Granada na Almeria zilikuwa zimetofautiana pointi nane na mabao matatu, hivyo kipigo kwa Granada na ushindi kwa Almeria inaweza kuleta mabadiliko kwenye sehemu hiyo ya mkiani kwenye msimamo wa La Liga. Cadiz yenyewe imekusanya pointi 33 kwenye mechi 37 na itabaki kwenye nafasi ya 18 na hivyo itashuka daraja, haitakuwapo kwenye La Liga msimu ujao.

Hata kwenye vita ya kusaka tuzo ya Pichichi, staa wa Villarreal, Alexander Sorloth ana nafasi kubwa ya kuingia baada ya kuingia mchezo wa mwisho wa msimu akiwa amefunga mabao 23, mawili zaidi ya mchezaji anayeshika nafasi ya pili, Artem Dovbyk wa Girona, aliyefunga mabao 21.

Wachezaji hao wawili, ndiyo wenye nafasi ya kunyakua Pichichi kwa msimu huu, huku kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham kuachwa mbali na mabao yake 19, atahitaji kufunga zaidi ya mara tano kwenye mchezo wa mwisho ili kupindua mechi na kubeba tuzo hiyo ya mfungaji bora kwenye La Liga kwa msimu huu wa 2023-24.

Chanzo: Mwanaspoti