Kocha Mkuu wa Tabora United, Masoud Djuma amesema kuwa timu yoyote iliyoko Ligi Kuu ya Tanzania inaogopa kukutana na timu ya Yanga kwa kuhofia kufungwa bao nyingi na kudhalilishwa.
Masoud amesema hayo jana baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la NBC dhidi ya Yanga ambapo Wananchi walitakata kwa mabao 3-0 na kutinga nusu fainali hiyo . “Acha tuwe wakweli tu, kucheza na timu ambayo inataka kushinda kila kitu sio kazi ndogo. Tumefungwa magoli rahisi sana lakini ndiyo hivyo wameshapita. Sisi tulikuwa kama tunajipima nguvu kuelekea mchezo ujao ambao ni wa mhimu zaidi kushinda huu wa leo (dhidi ya Yanga).
“Wakishakupanga na Yanga lazima uwe na hofu kwa sababu ni timu yenye wachezaji wazuri mmoja mmoja halafu wana muunganiko mzuri. Wapo kwenye wakati wao mzuri, lazima uzuie kwanza usije ukapigwa nyingi mapema.
“Plan yetu ilikuwa kuzuia kwanza tusishambulie haraka haraka, lakini haikuwezekana. Kipindi cha pili hizi bao mbili tumewapa, mtu anataka kupiga anampa mtu pasi. Ni makosa ambayo mchezaji anaweza kuyafanya lakini tumesahau hayo na sasa tunaangalia mechi ijayo.
“Tumepata nafasi kama mbili tatu lakini tukakosa utulivu wa kufunga, watu waliocheza mpira wanajua hii inaweza kutokea kwenye soka unapocheza na timu kubwa. Tumepeta nafasi hatujazitumia halafu wao tumewazawadia, unadhani hapo itakuwaje?
“Tumecheza vizuri kwa nidhamu, naamini tukicheza hivi dhidi ya Simba tunaweza kupata matokeo, tukikosa alama tatu tupate moja,” amesema Djuma.