Dirisha la majira ya baridi linakaribia nchini England. Timu nyingi zimeanza kufanya mazungumzo na baadhi ya mawakala wa wachezaji kuhakikisha wanapata mastaa ambao wataenda kuboresha vikosi vyao.
Kupiti tovuti ya The Mirro hapa tumekuletea uchambuzi wa mahitaji ya usajili kwa timu zote 20 za Ligi Kuu England ambayo zinaweza kuyatimiza kwenye dirisha hilo la Januari.
Arsenal - Ivan Toney
Licha ya uwepo wa Gabriel Jesus na Eddie Nketiah ambao wamekuwa wachezaji tegemeo kwenye kikosi cha Arsenal kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita ni wazi Arsenal wanamhitaji Toney ambaye wamekuwa wakimuwinda kwa muda mrefu.
Hii inatokana na kuumia mara kwa mara kwa Jesus na ubora ambao Toney aliuonyesha msimu uliopita.
Aston Villa - Beki
Wameonyesha maajabu msimu huu kwa kuwa kati ya timu zinazoshika nafasi sita za juu kwenye msimamp wa EPL.
Hawa wanahitaji kuboresha eneo lao la ulinzi kwa sababu beki wao tegemeo Tyrone Mings atakuwa nje kwa msimu mzima.
Bournemouth - Beki wa kati
Baada ya kuanza vibaya wamekuwa wakiimarika mechi hadi mechi. Hivi sasa wakiwa wametoka kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja.
Lakini rekodi yao ya kuruhusu mabao inaonyesha wanahitaji beki wa kati dirisha lijalo kwani kumekuwa na makosa mengi eneo hilo.
Brentford - Assane Diao
Brentford imepanga kuboresha eneo lao la ushambuliaji kwa dirisha lijalo kwa sababu huenda ikapoteza masta wake wawili tegemeo ambao ni Bryan Mbeumo na Ivan Toney, hapa wanadaiwa kutaka kumsajili winga wa Real Betis, Assane Diao.
Brighton & Hove Albion -Beki wa kushoto
Msimu huu Brighton imekuwa ikipitia changamoto ya majeraha kwenye kikosi chao. Hivi sasa vijana hawa wa Roberto de Zerbi wanamkosa beki wao wa kushoto Pervis Estupinan ambaye ni mmoja kati ya mastaa wao tegemeo, wachezaji walioonekana huenda wakaziba pengo lake nao wanasumbuliwa na majeraha. Katika dirisha lijalo kuna ziadi ya asilimia 70 wataingia sokoni kutafuta mbadala.
Burnley - Ian Maatsen
Vijana hawa wa Vincent Kompany wanahitaji kubadilika sana kuanzia mwakani ikiwa wanataka kuendelea kusalia kwenye ligi hiyo.
Moja ya maeneo ambayo yanawasumbua ni lile la ulinzi na kwa sababu hiyo wanadaiwa huenda wakamsajili Ian Maatseni ambaye aliwahi kucheza kwa mkopo kwenye timu yao.
Walijaribu kumsajili dirisha lililopita lakini alikataa. Kwa sasa hapati nafasi kubwa ya kucheza kwenye kikosi cha Chelsea.
Chelsea - Victor Osimhen
Kama kuna timu ambayo inalia sana na straika basi ni Chelsea, Christopher Nkunku amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha wakati Nicolas Jackson hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa.
Straika ambaye wamekuwa wakimuwinda tangu dirisha lililopita ni Victor ambaye hakuna ubishi juu ya kiwango chake.
Crystal Palace - Beki wa kulia
Wanahitaji kusuka kikosi chao kwenye maeneo mengi lakini zaidi ni beki wa kulia, Joel Ward amekuwa kwenye kiwango kibovu, Nathaniel Clyne ndio anazidi kuchuja wakati Nathan Ferguson naye akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Everton - Straika
Kipigo chao dhidi ya Manchester United wikiendi iliyopita kilionyesha ni jinsi gani wanahitaji mshambuliaji. Timu hii kutoka jijini Liverpool katika eneo la ushambuliaji inamtegemea zaidi Dominic Calvert-Lewin ambaye mara kadhaa amekuwa nje kutokana na majeraha, hivyo wakipata straika mpya huenda wakajiokoa kwenye janga la kushuka..
Fulham - Straika
Wamekuwa wakipitia wakati mgumu tangu wamuuze Aleksandar Mitrovic katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Tangu kuanza kwa msimu huu kwenye EPL wamefunga mabao 13 kwenye mechi 13. Wanahitaji mshambuliaji atakayeweza kuwapa mabao zaidi.
Liverpool - Kiungo wa kati
Kocha wao Jurgen Klopp alianza kazi ya kusuka upya eneo lao la ushambuliaji katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini licha ya kufanya hivyo bado kuna kazi ya ziada inatakiwa kufanyika kwani hadi sasa bado hawajapata mbadala wa Jordan Henderson na Fabinho.
Luton Town - Beki
Ni timu nyingine ambayo isipojiangalia itajikuta kwenye Championship msimu ujao. Vijana hawa wa Rob Edwards wanasumbuliwa na madhaifu kwenye maeneo mengi lakini eneo lao la ulinzi linaonekana kuhitaji maboresho zaidi.
Manchester City - Beki
Inawezekana ikawa si vyema kusema Man City wanahitaji maboresho na huenda wasitoe sana macho kwenye dirisha lijalo lakini kama kuna maeneo wanatakiwa wasajili basi lile la ulinzi ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likiruhusu sana mabao kwa msimu huu.
Manchester United - Straika
Umekuwa ni msimu ulioanza vibaya sana kwa Manchester United, licha ya kusajili kwa pesa nyingi katika dirisha lililopita wakimchukua staa kutoka Denmark Rasmus Hojlund kutoka Atlanta kwa Pauni 72 milioni, bado mashetani hawa wekundu wanaonekana kuhitaji straika kwenye eneo la ushambuliaji.
Newcastle United - Kiungo
Kusimamishwa kwa Sandro Tonali ina maana kwamba Newcastle lazima wapate mbadala wake ikiwa wanahitaji kuendelea kupambana vyema kwenye michuano mbali mbali. Hivyo ifikapo Januari moja ya maeneo yanayoonekana huenda wakayafanyia kazi ni hili.
Nottingham Forest - Straika
Umekuwa ni msimu wenye panda shuka kwa timu hii inayofundishwa na Steve Cooper. Kwa sasa straika wao Taiwo Awoniyi atakuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha. Wanahitaji mtu wa kuziba pengo lake.
Sheffield United - Beki wa kati
Wamekuwa na msimu mbaya. Beki wao wa kati Paul Heckingbottom anatajwa kuwa beki mwenye takwimu mbovu zaidi kwenye uzuiaji kwa msimu huu. Ili kujikwamua kwenye eneo la hatari mbali ya kuboresha maeneo mengine wanatakia kuweka sawa eneo hili.
Tottenham - STRAIKA
Mambo yalianza vizuri sana kwa vijana wa Ange Postecoglou mwanzoni wa msimu huu, lakini kwa sasa wanasumbuliwa na mzimu wa majeraha na James Maddison, Richarlison na Ivan Perisic wote wanaumwa na hiyo imesababisha wafanye vibaya kutokana na upungufu uliojitokeza kwenye eneo la ushambuliaji.
West Ham UNITED - MSHAMBULIAJI
Mbali ya uwepo wa Michail Antonio na Jarrod Bowen, taarifa zinadai kuna uwezekano wa Michail Antonio huenda akaondoka katika dirisha lijalo la majira ya baridi ama kiangazi. Kocha wao David Moyes anahitaji kumsajili mshambuliaji anayeweza kuwa mbadala wake.
Wolves - MSHAMBULIAJI
Chini ya Gary O’Neil, Wolves imekuwa ikifanya vizuri kwa msimu huu, hata hivyo licha ya ubora wao bado wanahitaji kusajili straika kuboresha eneo lao la ushambuliaji.