Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila mtu ashinde mechi zake EPL

Arsenal X Noyyingham Forest Kila mtu ashinde mechi zake EPL

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Arsenal imeonyesha kuwa siriazi kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kushinda mechi tano mfululizo na kuipa presha Liverpool kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.

Kwa sasa timu hizo zimetofautiana pointi mbili tu baada ya mechi 25. Liverpool inaongoza baada ya kukusanya pointi 57, Arsenal ipo kwenye nafasi ya pili, ikiishusha Manchester City baada ya kuvuna pointi 55.

Mabingwa watetezi Man City wenyewe wameporomoka hadi kwenye nafasi ya tatu, wakikusanya pointi 53, huku wakiwa wamecheza mchezo mmoja pungufu. Matokeo ya wikiendi yamekuwa na athari kubwa kwenye ligi hiyo.

VITA YA UBINGWA Man City imepoteza fursa muhimu ya kuongoza ligi endapo kama itashinda mchezo wake wa kiporo baada ya kubanwa mbavu na Chelsea katika mchezo uliofanyika uwanjani Etihad, Jumamosi iliyopita. Matokeo ya 1-1 dhidi ya Chelsea yameifanya Man City kubaki na pointi 53, ambapo hata kama watashinda kiporo chao, hawataweza kuwashusha Liverpool kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.

Arsenal imeichapa Burnley mabao 5-0 na hivyo kuzidi kuchochea moto kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, wakikomaa kwenye nafasi ya pili, pointi mbili tu nyuma ya Liverpool, ambao kama watateleza kwenye mchezo wao ujao, kisha Mikel Arteta na chama lake wakishinda, basi watakwea kileleni kwenye msimamo.

Kwa sasa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England zinatazamwa kama za farasi watatu, Liverpool, Arsenal na Man City, zikishushana zenyewe na timu ambayo itashindwa kujipanga vyema, basi itawekwa kando kwenye mbio. Liverpool imebaki kileleni baada ya kuichapa Brentford 4-1 katika mchezo wa Jumamosi.

TOP FOUR PATAMU Kabla ya mechi za wikiendi, Tottenham Hotspur ilikuwa kwenye nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 47 katika mechi 24. Aston Villa ilikuwa kwenye nafasi ya tano ikiwa na pointi 46.

Lakini, baada ya mechi za wikiendi, msimamo umebadilika, ambapo Aston Villa - ushindi wao wa mabao 2-1 ugenini huko Craven Cottage dhidi ya Fulham uliwafanya kuwaporomosha Spurs kwenye nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 49.

Spurs ilikubali kichapo kutoka kwa Wolves cha mabao 2-1 ikiwa nyumbani na hivyo kushika nafasi ya tano, pointi tatu tu nyuma ya Manchester United waliopo kwenye nafasi ya sita na pointi zao 44 baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Luton Town.

Kama ilivyo kwenye mbio za ubingwa, hata Top Four pia imekuwa vita ya timu tatu, ambapo tofauti ya pointi iliyopo hairuhusu kwa timu yoyote kupata matokeo ya hovyo, la itakuwa imekula kwao.

VITA YA KUSHUKA DARAJA Mechi ya wikiendi iliyopita kwenye Ligi Kuu England imeweka mwanga juu ya vita kali iliyopo kwenye timu zinazopambana kukwepa kushuka daraja. Hadi sasa vita hiyo inajumuisha timu saba, kuanzia inayoshika nafasi ya 14 kwenye msimamo kushuka chini.

Vita hiyo inahusu Brentford, Nottingham Forest, Crystal Palace, Luton Town, Everton, Burnley na Sheffield United.

Burnley na Sheffield United zimekabana koo mkiani kwenye msimamo wa ligi hiyo, kila timu ikiwa imekusanya pointi 13 katika mechi 25 na hali imekuwa mbaya baada ya kupoteza mechi zao za wikiendi iliyopita, ambapo vijana wa Vincent Kompany walikumbana na kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Arsenal, sawa na Sheffield United iliyopigwa 5-0 na Brighton.

Everton na Palace zenyewe zilitarajia kumenyana jana Jumatatu usiku, katika mechi itakayoamua namna zitakavyobadilishana nafasi kwenye msimamo. Ushindi kwa Palace itakayokuwa ugenini, itawaondoa kwenye kundi hilo, lakini kama Everton itashinda Goodison Park, basi itaishusha chini Luton, yenyewe ambayo ilikubali kichapo kutoka kwa Man United ikiwa nyumbani.

Kwenye vita hiyo ya kuwania kubaki kwenye ligi, timu zimetofautiana pointi chache sana, hivyo matokeo ya mechi zijazo yatakuwa na maana kubwa kwenye kutambua hatima yao baada ya mzunguko huo wa wiki ya 25 kwenye ligi hiyo.

BAADA YA WIKIENDI Vichapo tisa kati ya 14 ilivyokumbana navyo Luton kwenye Ligi Kuu England msimu huu vimekuwa vya tofauti ya bao moja tu, huku kukiwa hakuna timu iliyopoteza mechi nyingi kwa tofauti ya bao moja katika mikikimikiki hiyo msimu huu.

Nottingham Forest nao wamepoteza mechi tisa kwa staili kama hiyo. Man City na Arsenal pekee ndizo zilizoshinda mechi nyingi ugenini kuwazidi Man United msimu huu. Man City na Arsenal zenyewe zimeshinda mechi nane, wakati Man United imeshinda mechi saba ugenini, huku miamba hiyo inayonolewa na Erik ten Hag imeshinda mechi zote tatu za ugenini ilizocheza 2024.

Luton imefunga walau mara moja kwenye mechi zao 12 zilizopita kwenye Ligi Kuu England, ikiwa ni rekodi nzuri kwa timu iliyopanda daraja tangu Burnley ilipowahi kufanya hivyo kati ya Desemba 2016 na Machi 2017 (mechi 12 pia).

Kwa timu zilizopo kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Spurs ndiyo yenye rekodi ya walau kufunga bao moja kwenye mechi nyingi mfululizo, mechi 37.

Straika wa Man United, Rasmus Hojlund ameifungia timu hiyo bao la mapema kabisa kwenye Ligi Kuu England kwa mechi za ugenini, sekunde ya 37 tu na kuipa uongozi wa haraka wa mabao 2-0 timu yake hiyo kwenye mechi ya ugenini katika ligi baada ya dakika ya saba tu.

MECHI ZIJAZO Mchakamchaka wa Ligi Kuu England uraendelea leo Jumanne, ambapo Man City itakuwa nyumbani Etihad kukipiga na Brentford, wakati Liverpool itacheza kesho Jumatano na Luton Town huko Anfield kabla ya kufikia wikiendi, ambapo kutakuwa na mechi nyingi kuendeleza upinzani uliopo kwenye ligi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: