Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila la kheri Aisha Masaka England

Aisha Masaka England Kila la kheri Aisha Masaka England

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mtanzania Aisha Masaka juzi alikamilisha uhamisho wa kujiunga na timu ya wanawake ya Brighton inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya England ambayo msimu uliopita ilimaliza ikiwa nafasi ya 10.

Masaka amejiunga na Brighton akitokea BK Hacken ambayo mwaka 2022 alijiunga nayo akitokea Yanga Princess.

Kitendo cha Aisha Masaka kujiunga na Brighton kinamfanya kuwa Mtanzania wa pili kucheza daraja kubwa la ligi England akitanguliwa na Mbwana Samatta aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya nchi hiyo akiwa na Aston Villa.

Lakini pia Aisha Masaka anakuwa mwanasoka wa kwanza wa kike Tanzania kucheza soka la kulipwa katika Ligi Kuu ya Wanawake ya England.

Mafanikio ya Aisha Masaka ni jambo la kujivunia sana kwani yanatosha kuwa chachu kwa mabinti wa Kitanzania kupambana vilivyo ndani ya Uwanja waweze kufikia katika ngazi hizo au kuzikaribia.

Miaka minne tu iliyopita alikuwa anakimbizana kwenye viwanja vyetu na kusafiri kilomita nyingi kucheza mechi za ligi yetu lakini itakuwa tofauti na sasa ambapo anakwenda katika mazingira bora ya usafiri, mazoezi na huduma nyingine kwa mchezaji.

Atapata malisho ya kijani zaidi ambayo hapana shaka yatabadilisha hali yake ya kimaisha na pia kuwabadilisha wazazi, ndugu, jamaa na marafiki siku za usoni.

Kijiwe kinamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya huko England kwani akifanikiwa atasababisha kufunguliwa milango kwa mabinti wengi wa Kitanzania kuingia England au nchi nyingine barani Ulaya kwenda kutafuta maslahi bora zaidi ya yale wanayoyapata hapa.

Hongera nyingi kwa Aisha Masaka na tunamuombea apige hatua zaidi ya zile za sasa ili azidi kuitoa kimasomaso nchi.

Chanzo: Mwanaspoti