Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila la heri Simba kesho Misri

Simba X Ahly 2 2.jpeg Kila la heri Simba kesho Misri

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi, wawakilishi wa Tanzania katika mashindano mapya ya African Super League, Simba walizindua mashindano hayo kw akucheza na Al Ahly ya Misri katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kesho timu hizo zitakuwa zinarudiana katika Uwanja wa Al Salam jijini Cairo.

Itakumbukwa kwamba katika mchezo wa juzi uliopigwa Dar es Salaam uliokuwa wa uzinduzi wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza barani Afrika, ulishuhudiwa ugeni mkubwa kutoka katika 'familia' ya soka duniani, ikiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) Gianni Infantinho ulishuhudia ukaribu wetu katika ardhi ya Tanzania.

Ni katika tukio hilo, pia kiongozi huyo na vigogo wenzake wa mpira wa miguu duniani waliishuhudia Simba ikimaliza dakika 90 za mchezo huo ikitoka sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pamoja na mambo mengi yaliyoshuhudiwa katika mchezo huo, lakini kiwango cha soka cha wawakilishi hao wa nchi kilionyesha kuwapa matumaini mashabiki wao kutokana na namna wachezaji walivyojituma hasa kuanzia kipindi kile cha pili.

Ni wazi kwamba kama usingekuwa uzembe uliojitokeza katika kipindi hicho baada ya Simba kurejea kutoka nyuma ilipofungwa bao hadi mapumziko na kuja kuongoza kwa mabao 2-1, basi timu hiyo ingeondoka na ushindi na kuwapa raha ya pekee mashabiki wake.

Hata hivyo, katika soka lolote linaweza kutokea na ndicho kilichotokea kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ambayo inaipa nafasi kila timu kufuzu nusu fainali ya mashindano hayo ambayo yanatajwa kuwa na fedha nyingi kwa timu shiriki.

Wakati tukiipongeza Simba ambayo kabla ya mchezo huo kila mmoja alikuwa haipi nafasi ya kushinda, tunawaomba viongozi hususan benchi la ufundi wacheze vyema karata ili kuibuka na ushindi jijini Cairo ikizingatiwa kwamba hawana muda mrefu wa maandalizi.

Kimsingi kilichopo mbele yao ni kupangilia vyema kikosi kitakachoanza katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu na wa pekee kwa timu hizo na hasa kwa kuwa timu kutoka nchi za Afrika Kaskazini hubadilika zaidi kimchezo zinapokuwa katika ardhi ya nchi zao.

Ni kwa msingi huo, Simba inapaswa kujipanga barabara kuanzia nje ya uwanja eneo ambalo timu za mataifa hayo huanzia kuwakatisha tamaa wapinzani wao kabla hata ya mchezo na kumalizana nao uwanjani wakati wa mechi ambako figisu pia nyingi.

Hata hivyo tunaamini kwamba kwa kuwa Simba ni miongoni timu nane tu Afrika zinazoshiriki mashindano hayo kutokana na ubora ziliouwekeza kwa miaka mingi, timu hiyo inajua namna nzuri ya kukabiliana na changamoto zote za ugenini ili kufikia lengo ililokusudia.

Kwa wapenzi na Watanzania kwa ujumla ni vyema nao wakajivika jukumu la kuiombea ili ipeperushe vyema bendera ya nchi katika nchi ya kigeni kwa sababu mafanikio itakayoyapata katika mchezo huo na mingine iliyo mbele yake yanaifanya nchi iheshimike zaidi.

Kama ilivyokuwa katika mchezo wa juzi, ni vyema mashabiki wa soka kwa pamoja wakaungana katika hili, ikizingatiwa pia kwamba ni Al Ahly hii hii inayorejea tena nchini kwa ajili yam mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga, hivyo ni vyema tuwaonyeshe Watanzania tuko kitu kimoja kwa timu zetu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: