Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila la Heri Taifa Stars Chan 2021

51d3517537b64879bec57c26956a1eec Kila la Heri Taifa Stars Chan 2021

Sun, 17 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

FAINALI za sita za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka la nyumbani (Chan) zinaanza leo nchini Cameroon na Tanzania ni miongoni mwa nchi 16 zilizofuzu hatua hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushiriki fainali hizo za Chan baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2009 nchini Ivory Coast wakati Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) lilipoyaandaa kwa mara ya kwanza.

Tanzania iliposhiriki fainali za mwaka 2009 ilipangwa katika Kundi A pamoja na Zambia wenyeji Ivory Coast na Senegal na kumaliza katika nafasi ya tatu katika hatua ya makundi na hivyo kushindwa kutinga hatua inayofuata.

Katika mashindano hayo, Tanzania iliifunga Ivory Coast na kutoka sare ya 1-1 na Zambia, lakini ilijikuta ikifungwa 1-0 na Senegal katika hatua hiyo.

Mwaka huu Taifa Stars, ambayo imecheza mchezo mmoja wa majaribio dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kutoka suluhu, iko kundi moja na Zambia, Namibia na Guinea.

Timu yetu imeondoka ikiwa salama haina matatizo yoyote, kwani Serikali ilitoa kiasi cha Sh milioni 60 kwa ajili ya posho za ndani za wachezaji pamoja na bonasi ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hatua hiyo ya Serikali ni utekelezaji wa ahadi zake za kusaidia timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa ili kuzipunguzia mzigo na kuziwezesha kujiandaa vizuri zaidi.

Ni matarajio ya wengi kuwa Taifa Stars itafanya vizuri na kuweka rekodi ya kucheza kwa mara ya kwanza hatua ya robo fainali ikizidi mara ya kwanza tulipoishia makundi katika Chan 2009, na Afcon 1980 ma 2019 Nigeria na Misri.

Wachezaji Taifa Stars wanatakiwa kujituma zaidi na kujua kuwa nyuma yao kuna zaidi ya watu milioni 50 wakiwafuatilia kwa karibu kuona watavuna nini huko Cameroon.

Hiki ni kipindi muafaka kwa wachezaji wetu kuonesha uzalendo kwa nchi yao kwa kuipigania kwa nguvu zote bendera yetu ya taifa, ambayo itakuwa ikipepea Cameroon wakati wote wa mashindano hayo.

Kufanya vizuri kwa Stars Chan kutawatia moyo zaidi wachangiaji wa timu hiyo kuwa na imani zaidi na timu yao na kuichangia zaidi sio tu katika mashindano hayo, ila na hata mengine.

Wachezaji wa Taifa Stars wayatumie mashindano hayo kutangaza majina yao ili waweze kupata timu za kucheza nje ya nchi kama kwa Mbwana Samatta, Simon Msuva na wengine, ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi baada ya kufanya vizuri nchini.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa makusudi liliamua kuanzisha mashindano hayo ili kuhakikisha wachezaji wanaocheza soka katika ligi zao za nyumbani, nao wapate fursa ya kuonekana nje ya nchi zao na ikiwezekana nao wachukuliwe.

Yote na yote tunawatakiwa heri wachezaji wetu wafanye vizuri Chan 2021 Cameroon.

Chanzo: habarileo.co.tz