Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikoti, mtambo wa mabao Namungo unaomuota Yondani

77944 Kikoti+pic

Tue, 1 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lucas Kikoti wa Namungo ya Lindi, ameanza kuwa gumzo licha ya uchanga wake katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Mchezaji huyo ameanza kutema cheche baada ya kufunga mabao mawili akishika nafasi ya pili nyuma ya Meddie Kagere wa Simba aliyefunga matano.

Kiwango bora cha Kikoti kimeanza kutia nafasi za washambuliaji wakongwe katika Ligi Kuu katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu.

Msimu uliopita Kikoti alishika nafasi ya pili kwa kufunga mabao akifunga tisa nyuma ya pacha wake anayecheza naye Namungo Reliants Lusajo aliyefunga 15 katika Ligi Daraja la Kwanza. Mchezaji huyo anasema anataka kutimiza ndoto yake ya kutwaa kiatu cha dhahabu katika Ligi Kuu msimu huu.

Hata hivyo, anasema haitakuwa kazi nyepesi kwake kwani ligi hiyo ina mabeki katili kama Kelvin Yondani ambaye anakiri ni mchezaji anayemnyima usingizi.

Akizungumza na Spoti Mikiki, Kikoti anasema Yondani ni beki katili ambaye hatamsahau walipokutana wakati huo akiwa mchezaji wa Majimaji ya Songea kabla ya timu hiyo kuteremka daraja.

“Yondani ni beki katili sana hawezi kukuruhusu kirahisi umpite lakini kwa mabeki wengine wamekuwa wakicheza kwa nidhamu sana. Yondani anaweza kukufanyia kitendo ambacho hata mwamuzi anaweza asione, lakini nimekuwa nikitumia mbinu mbadala kukabiliana naye. “Niliwahi kukutana naye kwa mara ya kwanza nikiwa Majimaji ni beki ambaye unatakiwa kutumia mbinu kukabiliana naye,” anasema Kikoti.

Pia Soma

Advertisement
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu, Namungo itacheza na Yanga Februari 26 kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Kikoti anamtaja Yondani licha ya kuwemo mabeki wengine wa kati wazoefu kina Aggrey Morris wa Azam, Pascal Wawa na Erasto Nyoni wanaocheza Simba.

Kikoti anasema atashindana na wakongwe kina Kagere kuwania tuzo ya ufungaji bora kwa kuwa uwezo wa kufunga mabao anao.

Katika mechi ambazo Namungo imecheza Kikoti ameonyesha ni mchezaji mwenye kiwango cha kufika mbali katika soka.

Kocha wa Namungo, Thiery Hitimana anasema Kikoti ndiye tegemeo lake katika safu ya ushambuliaji akishirikiana na Lusajo.

“Kwanza nimeshangaa kwanini hayumo katika kikosi cha Taifa Stars, Kikoti ni mshambuliaji mwenye uwezo mzuri wa kufunga mabao ana sifa za kucheza timu ya Taifa,” anasema Hitimana raia wa Burundi.

Kikoti aliyeanza kucheza soka akiwa Shule ya Msingi Huduma wilayani Songea, anasema kipaji chake kiliibuliwa na Kocha Ramadhani Mkono.

“Siwezi kumsahau Mkono kwa sababu kama ningekuwa naenda kwa wazazi wangu ingekuwa ngumu kuninunulia viatu, alikuwa na ushawishi. Kocha mwingine ambaye nitamkumbuka ni Kali Ongala,” anasema.

Kwa nini Kali? Kikoti anasema ni kocha ambaye akiwa Majimaji kama mchezaji wa kujitolea alimuamini na kumpa nafasi ya kucheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.

“Ilikuwa mwaka 2012 nilianzia timu B ya Majimaji ndani ya msimu wangu wa kwanza lakini hapo tulikuwa na kocha mzungu kabla ya kuja Kali ambaye alinipa nafasi ya kucheza Shinyanga na Kagera Sugar, niliingia kipindi cha pili nilifurahi kwasababu nilianza kuona ndoto yangu inaanza kutimia,”anasema Kikoti.

Hata hivyo anasema ndoto yake nusura iingie doa baada ya basi lao kutaka kutumbua ziwani wakiwa njani kurejea Songea wakitokea Kagera.

Anasema aliitosa Majimaji aliyocheza misimu mitatu baada ya kushuka daraja na kujiunga na Namungo ambayo aliisaidia kupanda Ligi Kuu msimu uliopita.

“Ligi Kuu ni tofauti na daraja la kwanza hilo nalitambua lakini hii sio mara yangu ya kwanza kucheza. Najua kuwa Kagere ni mchezaji mzuri ila nitajitahidi kuzitumia nafasi ambazo nitakuwa nikipata,” anasema Kikoti.

Licha ya kuwa ni kiungo mshambuliaji ambaye mara kadhaa kupangwa kama namba 10, anaamini anaweza kutimiza ndoto hiyo kwa kuwa ana kipaji cha soka.

Akizungumzia klabu za Simba na Yanga, mshambuliaji huyo anasema soka ni kazi yake hivyo atakuwa tayari kuzitumikie endapo pande zote zitafikia mwafaka.

“Soka ni kazi yangu siwezi kusema nitajiunga na Simba au Yanga. Jambo la msingi ni mwafaka wa pande zote ili kuepusha mkanganyiko,” anasema Kikoti.

Pia Kikoti anasema pamoja na kutaka kiatu cha dhahabu, anataka kucheza timu ya Taifa ili kutoa mchango wake.

“Sijakata tamaa, naamini nafasi ya kuitwa timu ya Taifa ipo na muda ukifika itakuwa hivyo. Napenda kutoa mchango wangu kwa Taifa Stars kwasababu naamini nina uwezo wa kufanya hivyo,” anasema mshambuliaji huyo mfupi wa wastani, lakini mwenye kasi ya kupambana na mabeki. Namungo ina pointi saba katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Chanzo: mwananchi.co.tz