Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikosi cha mastaa 11 waliolimwa kadi nyekundu Ligi Kuu

Mastaa 11 Kikosi cha mastaa 11 waliolimwa kadi nyekundu Ligi Kuu

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kufikia Jumatatu ya wiki hii, wachezaji 12 kutoka timu 12 walikuwa wamepata kadi nyekundu kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

Timu za Simba, Azam FC, Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar ndizo pekee zilikuwa hazina mchezaji ‘aliyekula umeme’ hadi sasa.

Wachezaji 12 waliolimwa kadi nyekundu ukiwaweka pamoja wanatosha kuunda kikosi kimoja matata kabisa ambacho kinaweza kuwasha moto kwenye Ligi Kuu Bara. Kupitia makala haya Mwanaspoti linakuletea ‘chama’ la kadi nyekundu Ligi Kuu 2023-24.

METACHA MNATA (YANGA)

Huyu ni kipa wa Yanga, alipata kadi nyekundu Februari 11, mwaka huu baada ya kumdaka, Samson Mbagula wa Tanzania Prisons dakika ya 57.

Mechi hiyo ilimalizika kwa Yanga kushinda 2-1 kwa mabao ya Clement Mzize na Pacome Zouzoua huku lile la Prisons likifungwa na Jeremiah Juma.

MWAITA GEREZA (GEITA GOLD)

Mbavu ya kulia atasimama staa huyu wa Geita Gold. Mwaita anayemudu kucheza beki ya kulia alipata kadi nyekundu Oktoba 21, mwaka jana kwenye mechi ya ligi ambapo timu hiyo ilikuwa nyumbani kuikaribisha Dodoma Jiji.

Kadi hiyo ilitokana na Mwaita kumchezea faulo mbaya, Emmanuel Martin dakika ya 73 ya mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mabao ya Geita yalifungwa na Tariq Seif na Hassan Mahamoud huku yale ya Dodoma Jiji yote mawili yakifungwa na Hassan Mwatarema.

KENETH KUNAMBI (IHEFU)

Beki huyu wa Ihefu mwenye uwezo wa kucheza nafasi tofauti katika eneo hilo alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kudaka mpira dakika ya tatu ya mechi dhidi ya Namungo iliyopigwa Novemba 23, mwaka jana na kuisha kwa Namungo kushinda 2-0.

Mabao ya Namungo katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi yalifungwa na Pius Buswita na Hamad Majimengi.

JORAM MGEVEKE (DODOMA JIJI)

Mgeveke anayekipiga Dodoma Jiji alionyeshwa kadi nyekundu Novemba 29, mwaka jana katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambapo wenyeji walishinda bao 1-0, lililofungwa na Jumanne Elifadhili kwa penalti.

Kadi hiyo ilitoka baada ya Mgeveke kumchezea faulo aliyekuwa winga wa Prisons, Edwin Balua ambaye kwa sasa yupo Simba.

ABDALLAH MFUKO (KAGERA SUGAR)

Huyu ni beki mzoefu anayekipiga Kagera Sugar na alipata kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Ihefu iliyopigwa Februari 25 mwaka huu baada ya kumchezea madhambi mshambuliaji wa Ihefu Mkenya, Elvis Rupia.

Hata hivyo, kadi hiyo haikuiathiri Kagera kwenye mchezo huo kwani mechi ilimalizika kwa kushinda 2-1, kwa mabao ya Obrey Chirwa na Dickson Mhilu huku lile la Ihefu likifungwa na Tchakei aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Singida Fountain Gate.

ABDUMALIK ZAKARIA (NAMUNGO)

Huyu ni kiraka wa Namungo aliyeonyeshwa kadi nyekundu Oktoba 4, mwaka jana kwenye mechi ya Ligi dhidi ya Kagera Sugar katika dakika ya 78.

Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ulimalizika kwa sare ya mabao 1-1 Kagera ikitangulia kwa bao la Ally Nassor dakika ya 34 kisha Namungo kuchomoa dakika ya 72 kupitia kwa Pius Buswita.

HAJI UGANDO (COASTAL UNION)

Winga huyu wa Coastal Union alipata kadi nyekundu kwenye mechi ya duru ya tatu dhidi ya Simba baada ya kumkanyaga beki, Henock Inonga wa Simba dakika ya 19 ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru Septemba 21, mwaka jana.

Katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 3-0 na yote yakifungwa na Mkongomani, Jean Baleke ambaye ameachana na kikosi hicho.

MASSOUD ABDALLAH ‘CABAYE’ (KMC)

Namba nane anasimama huyu kiungo wa KMC aliyekuwa wa kwanza kupata kadi nyekundu msimu huu katika duru ya tatu akicheza dhidi ya JKT Tanzania, Septemba 15, 2023.

Cabaye alitolewa katika dakika ya 90 ya mchezo huo baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano katika mechi iliyomalizika kwa KMC kushinda 2-1, kwa mabao ya Awesu Awesu na Wazir Junior huku lile la kufutia machozi kwa JKT likifungwa na Edward Songo.

HASSAN MWATEREMA (DODOMA JIJI)

Straika huyu wa Dodoma Jiji alilimwa kadi nyekundu Februari 15, mwaka huu baada ya kumkanyaga beki wa Coastal Union, Lameck Lawi.

Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ulimalizika kwa wenyeji Coastal kushinda 1-0, kwa bao la Ibrahim Ajibu la penalti.

HASSAN NASSORO ‘MACHEZO’ (JKT TZ)

Namba 10 anasimama huyu kiungo wa JKT Tanzania aliyekula umeme Desemba Mosi mwaka jana kwenye mechi dhidi ya Singida Fountain Gate iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Machezo alipata kadi hiyo licha ya kukifungia kikosi hicho bao na jingine likifungwa na Hassan Kapalata huku yale ya Singida yakifungwa na Francy Kazady na nyota wa zamani, Marouf Tchakei ambaye kwa sasa anakipiga kwenye klabu ya Ihefu.

MORICE CHUKWU (SINGIDA FG/IHEFU)

Kiungo huyu Mnigeria anayekipiga kwa sasa Ihefu, alionyeshwa kadi nyekundu Desemba Mosi mwaka jana wakati akiichezea Singida Fountain Gate katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania ulioisha kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

AKIBA ‘SUB’:

NGELEKA KATEMBUA (KAGERA SUGAR)

Huyu ni kipa wa Kagera aliyeonyeshwa kadi nyekundu Desemba 9, mwaka jana kwenye mechi dhidi ya Coastal Union baada ya kumtwanga ngumi mchezaji wa Coastal na kuifanya timu hiyo kupoteza kwa bao 1-0, lililofungwa na Charles Semfuko.

Chanzo: Mwanaspoti