Manchester United itafanya usajili wa nguvu kipindi hiki cha majira ya ngazi endapo wawekezaji kutoka Qatar watakamilisha mchakato wa kuinunua klabu hiyo.
Mkongwe wa klabu hiyo Rio Ferdinand alidai kwamba Sheikh Jassim ndiye atakuwa mmiliki mpya wa Man United kwani mchakato upo katika hatua nzuri.
Endapo wawekezaji hao kutoka Qatar watafanikiwa kuinunua Man United kwa Pauni 5.5 Bilioni, basi watatoa pesa ndefu katika usajili wa dirisha la kiangazi na kocha Erik ten Hag atafaidika zaidi.
Man United imehusishwa na wachezaji wengi kipindi hiki cha usajili kwasababu wanataka kuimarisha kikosi kwaajili ya maandalizi ya msimu ujao. Lakini kuna baadhi ya madili ambayo yamekwama kutokana na mkwanja.
Man United wamehusishwa na wachezaji wawili wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe na Neymar - ambao wote wameweka wazi kwamba kuna uwezekano wakaondoka katika dirisha hili la usajili.
Mbappe, 24, amehusishwa na Real Madrid na Chelsea na klabu nyingine kutoka Saudi Arabia ambazo zinanyemelea Neymar. Lakini kwa upande wa Man United ingependa kuwasajili wote kama wanataka kuboresha kikosi chao na kuleta ushindani kwenye ligi.
Wengine wanaotajwa ambao wanawindwa na Man United ni kipa wa Porto, Diogo Costa ambaye anapendekezwa akachukue nafasi ya David de Gea. Hiyo ni baada ya kukosa saini ya kipa wa Brentford, David Raya.
Beki mwingine aliyehusishwa anatokea Napoli, Kim Min- Jae na huenda akashirikiana na Lisandro Martinez katika safu ya ulinzi msimu ujao.
Casemiro na Bruno Fernandes wanatarajia kuunda safu ya kiungo na Mason Mount, 24 endapo dili litiki. Man United inajipanga kuongeza ofa baada ya Pauni 40 milioni walizotoa kukataliwa na The Blues. Hata hivyo bado wanaamini kiungo huyo atatua mitaa ya Old Trafford.