Hakika ulikuwa msimu wa aina yake huku wakishuhudiwa watani wa jadi, Simba na Yanga wakiendelea kutesa kwenye mbio za ubingwa ambao Wananchi wameutetea, lakini pia ilishuhudiwa Singida BS ikiibuka na kufanya makubwa licha ya ugeni wao na kumaliza kwenye nafasi nne za juu.
Kwa Masau Bwire na Ruvu Shooting yake jahazi lao lilizama wiki chache kabla ya msimu kumalizika, hakuna ambaye alionekana kuwaza kuwa wanaweza kushuka daraja mwanzoni mwa msimu kutokana na uzoefu wao lakini kadiri ambavyo walikuwa wakipoteza pointi ndivyo mambo yalivyowaendea kombo.
Maafande wa Tanzania Prisons walitusapraizi mwishoni mwa msimu kwani wapo ambao waliamini wangekuwa miongoni mwa timu ambazo zitashuka daraja, lakini walijinasua kwenye hatari hiyo na kusogea hadi katikati mwa msimamo wakiwa chini ya kocha Mzanzibar, Abdallah Mohamed.
Licha ya uwepo wa hayo yote na mengine kibao ambayo tuliyashuhudia msimu huu, hiki hapa kikosi cha wachezaji 11 ambao wamekuwa kwenye viwango bora kwa kuzingaria takwimu zao, kikosi hiki kimepangwa kwa mfumo wa 4-5-1.
DJIGUI DIARRA
Yanga ni miongoni mwa timu ambazo zimeruhusu mabao machache zaidi kwenye ligi, hiyo inadhihirisha ubora wa Diarra pamoja na ukuta wake.
Diarra ndiye kipa ambaye anaongoza kucheza michezo mingi (16) bila ya kuruhusu bao huku akifuatiwa na Aishi Manula ambaye alikosa michezo ya mwishoni mwa msimu kutokana na kusumbuliwa kwake na majeraha ya nyonga.
Kipa huyo wa Kimataifa wa Mali, amekuwa na muendelezo wa kiwango ubora kwani msimu uliopita alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao waliunda kikosi cha msimu huku akicheza bila ya kuruhusu bao kwenye michezo 15.
Diarra amekuwa midomoni mwa mashabiki wengi wa Yanga mbali na uwezo wake wa kuokoa michomo lakini pia ni mzuri wa kuanzisha mashambulizi jambo ambalo linamtofautisha na makipa wengi wa kigeni ambao wamepita nchini.
SHOMARY KAPOMBE
Japo amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya hapa na pale, amekuwa na msimu mzuri ukilinganisha na Djuma Shaaban wa Yanga ambaye alipoteza ubora wake mwishoni mwa msimu kiasi cha kusugua benchi mbele ya Dickson Job.
Kapombe ameifanya Simba kuwa na nguvu ya ziada wakati wa kujenga mashambulizi yake, amekuwa akiongeza namba ya wachezaji kwenye kushambulia jambo ambalo limekuwa likiwapa wakati mgumu wapinzani wao.
Wakati ambao Simba imekuwa ikishambuliwa hurejea kwa haraka katika nafasi yake kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya msingi kama beki.
MOHAMMED HUSSEIN
Anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wamecheza michezo mingi zaidi kwenye ligi, ni mzuri kwenye kushambulia na kuzuia kama ilivyo kwa Kapombe.
Zimbwe Jr ni mchezaji kiongozi ambaye licha ya kuwa nahodha msaidizi amekuwa akitekeleza majukumu hayo kwa kiasi kutokana na John Bocco kutopata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.
Beki huyo wa kushoto amekuwa bora kipindi kile ambacho Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara misimu minne mfulilizo hadi sasa, ikumbukwe kuwa msimu uliopita alikuwa kwenye kikosi bora cha msimu ambacho kilitolewa na TFF.
DICKSON JOB
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amekuwa na mabadiliko mengi kwenye kikosi chake kuna kipindi alimweka nje Bakari Mwamnyeto kabla ya kurejea kwenye kiwango chake lakini Job aliendelea kutumika kwenye kikosi cha kwanza hata kwenye nafasi ambazo hakuzoeleka kucheza kutokana na mahitaji ya timu.
Job ndiye beki bora kwa Yanga mbali kuibuka kwa Ibrahim Bacca mwishoni mwa msimu ambapo alionyesha kiwango cha juu, jamaa amekuwa akiupiga mwingi kiasi cha kuwa msaada upande wa beki ya kulia ambayo ilionekana kulegalega.
Kiasi Job sio beki wa pembeni eneo ambalo huwa anatumika Shaaban Djuma lakini amekuwa msaada hasa kwenye michezo ambayo Nabi alitaka kuwa ukuta imara huku upande wa kushoto akicheza Kibwana Shomary badala ya Joyce Lomalisa.
HENOCK INONGA
Ni beki kisiki kwelikweli ambaye ameifanya Simba kuwa na ukuta imara sambamba na Joash Onyango.
Kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita ambapo aliingia kwenye kikosi bora cha msimu cha TFF hakuna shaka kuwa anaweza kuendelea kuwa sehemu ya kikosi hicho kwa msimu mwingine tena kutokana na ubora wake.
MZAMIRU YASSIN
Msimu uliopita ulikuwa wa Yannick Bangala ambaye hakuwa akishika kwenye ligi hasa kwenye eneo la kiungo cha chini lakini awamu hii, Mzamiru Yassin anaonekana kuwa kwenye kiwango bora zaidi.
Bila shaka nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, anaweza kumpiga bao kwa msimu huu, Sadio Kanoute ambaye amekuwa akikumbana na adhabu ya kadi.
SAIDO NTIBAZONKIZA
Alianza kuonyesha makali yake msimu huu akiwa na Geita Gold kabla ya Simba kumnyakua kwenye dirisha dogo na kuwa msaada kwenye kikosi chao.
Nyota huyo wa zamani wa Yanga, ni miongoni mwa wachezaji wa Simba wenye mabao mengi (10) zaidi kwenye ligi. Ni mzuri kushambulia hasa akitokea pembeni licha ya kuwa na uwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji.
BRUMO GOMES
Licha ya ugeni wake kwenye ligi ameonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kumezewa mate na klabu mbalimbali kubwa Ligi Kuu Bara, ikiwemo Yanga.
Gomes mwenye mabao tisa kwenye ligi, ni fundi wa mipira ya adhabu. Kiungo huyo ameinogesha Singida BS kwenye eneo la kiungo kutokana na ubunifu alionao.
FISTON MAYELE
Ameonyesha kwa kiwango kikubwa namna anavyolijua goli, ameifanya Yanga kuwa tishio, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa DR Congo amefunga karibu kila aina ya bao kwenye viwanja mbalimbali na ndiye mfungaji bora wa ligi.
Mayele amekuwa gumzo Afrika kiasi cha kunyemelewa na klabu mbalimbali kubwa barani Afrika kutokana na kuwa mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na mabao saba ambayo yamechangia Yanga kufika fainali.
CLATOUS CHAMA
Ukiongelea wapishi wa mabao basi lazima umtaje Mwamba wa Lusaka, Clatous Chama mwenye asisti 14, ameonyesha ubora wa aina yake.
Fundi huyo ambaye alianza likizo yake mapema kutokana na kuwa na adhabu, ni kati ya wachezaji bora wa kigeni kwenye soka la Tanzania.
SIXTUS SABILO
Takwimu zake zinatisha, nyota huyo wa Mbeya City ni kati ya wachezaji wachache kwenye ligi ambao wamehusika na mabao mengi. Amefunga mabao tisa na kutoa asisti saba.
KOCHA: NASREDDINE NABI
Mashabiki wa Yanga hawamdai Nasreddine Nabi kutokana na kile ambacho amefanya kwenye klabu yao kwa msimu wa pili mfululizo kuanzia kwenye ligi hadi upande wa kimataifa licha ya kwamba kipindi fulani alikumbana na changamoto ambazo ilibaki kidogo tu afungashiwe virago vyake huko Jangwani.