Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikao cha wachezaji Simba chaibua mapya

98563 Kikao+pic Kikao cha wachezaji Simba chaibua mapya

Tue, 10 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simba kesho Jumatano wanawakaribisha vibonde wa Ligi Kuu Bara, Singida United kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam lakini kikao cha wachezaji na viongozi baada ya mechi ya Yanga kimebaini mambo mapya ya kuyafanyia kazi kwa haraka.

Uongozi wa mabingwa hao watetezi umesema kufungwa bao 1-0 na Yanga hakuzuii wao kutwaa ubingwa na kikubwa wanachokifanya ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji wao kuifuata mechi hiyo na nyingine nane zilizobaki ukiondoa ya kesho.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Baada ya mechi, kama viongozi tulizungumza na wachezaji wetu ambao walionekana kuathirika kisaikolojia na matokeo hayo, hivyo jambo la kwanza ni kuwajenga kisaikolojia ili wasiharibu zaidi mechi zijazo.”

“Tunacheza na Singida, tunahitaji kushinda hiyo, nimewaeleza kwamba wanapaswa kusahau matokeo hayo ili wawe sawa mchezo ujao ingawa nafahamu kwamba mashabiki wanahitaji matokeo mazuri ila kwenye michezo hasa ya dabi lazima kukubaliana na matokeo ya aina yoyote.

“Hizi mechi zinakuwa na presha kubwa na kila timu inahitaji ushindi hivyo lolote linaweza kutokea. Hata ukiangalia tumecheza vizuri ila matokeo mazuri wamepata wapinzani wetu, tunapaswa kuwapongeza pia,” alisema na kuongeza

“Furaha ya mashabiki ni ushindi hivyo tunawaahidi kufanya vizuri katika mechi zilizobaki na kutwaa ubingwa, pia tumewaeleza benchi la ufundi kuendelea kuwajenga wachezaji ili wasitoke mchezoni tunaamini hili litafanikiwa,” alisema Senzo.

Pia Soma

Advertisement
Mbali na kuwajenga kisaikolojia wachezaji wao, pia uongozi umewataka wanachama na mashabiki wao kutokata tamaa na matokeo hayo kwani lengo lao halijafeli ambalo ni kuchukuwa ubingwa wa ligi pamoja na Kombe la FA.

Simba wanaingia kuwakabili Singida United ambao tayari hali yao ni tete kwani wanashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamekusanya pointi 12 pekee katika mechi 27 walizocheza ambazo ni sawa Simba waliovuna pointi 68.

Wakati Simba wakiwa nyumbani, Tanzania Prisons nayo itawakaribisha Alliance Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya hapo kesho.

Katika msimamo Prisons wapo nafasi ya 11 wakiwa na pointi 37 huku wapinzani wao wanashika nafasi ya 15 kwa pointi 29, timu zote zimecheza mechi 27 hadi sasa.

Chanzo: mwananchi.co.tz