Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa uongozi wa kampuni yake ya Hk Group umekamilisha makubaliano na wawekezaji hivyo kwa sasa unaweza kununua hisa ndani ya Simba Sc ama Yanga Sc.
Kigwandalla ambaye ni shabiki na mwanachama wa Simba Sc ametoa kauli hiyo leo kupitia ukurasa wake wa Twitter ikiwa ni siku moja baada ya Mwekezaji wa Simba Sc, Mohammed Dewji kudai kuwa anafikiria kukata tamaa baada ya mchakato wa mabadiliko wa klabu hiyo kukwamba kwa miaka sita sasa.
"Hatimaye menejimenti ya HK Group na wawekezaji wenza wawili (consortium) imekamilisha makubaliano na sasa itakuwa tayari kununua hisa na kuwekeza kwenye timu ya Yanga SC ama Simba SC, kama fursa itakuwa wazi na ama mwaliko utatolewa!," ameandika Kigwangalla.
Ikumbukwe kuwa, Kigwangallah na Mo Dewji waliwahi kutibuana kisa sakata hilo la uwekezaji ndani ya Simba Sc huku Kigwangalla akimtuhumu mfanyabiashara huyo kutolipa Tsh bilioni 20 alizoahidi kwa Yanga kama gharama ya kununua hisa asilimia 49 ya uwekezaji.