Umepita mwaka mmoja na ushei tangu sakata la Bernard Morrison alipokuwa Yanga kutua Simba baada ya kuwazidi akili mabosi wa Yanga kwenye kesi iliyofunguliwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kabla ya kesi kuhamia CAS na kutolewa hukumu mwaka jana.
Licha ya muda mrefu kupita tangu sakata hilo kumalizika, lakini mtu aliyebebeshwa mzigo wa kuhukumu kesi hiyo ndani ya TFF kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, imebaki kumbukumbu isiyofutikwa kichwani mwa aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Elias Mwanjala.
Mwanjala amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi juu ya kesi hiyo na namna ilivyoweza kumlaza nje ya nyumba yake kwa siku kadhaa ili kuitatua baada ya nyota huyo kusaini Simba huku Yanga wakidai bado ni mchezaji wao kwa madai kwamba alikuwa amesaini mkataba mpya.
Anabainisha kesi hiyo ilikuwa na vitu vingi, huku vingine vilikuwa nje ya uwezo wake, lakini alijitahidi kuhakikisha anafanya uamuzi kwa kufuata haki licha ya kuwa ni Yanga lialia.
Anakiri huenda kesi hiyo ndiyo iliyomfanya akapigwa rungu la kufungiwa miaka miwili kujihusisha na soka kwa kuwa Uchaguzi wa TFF ulikuwa Septemba, huku yeye akifungiwa Desemba akihoji kwa nini baada ya kesi ya Morrison afungiwe wakati uchaguzi ulishafanyika. Ebu endelea naye...!
SAKATA LA MORRISON
Mwanjala anasema aliwahi kupitia kesi mbalimbali akiwa ndani ya kamati hiyo, lakini kesi ya Morrison baada ya kusajiliwa Simba ilikuwa ngumu na ilimfanya kupata maadui kutoka Yanga timu anayoipenda katika maisha yake.
“Ile kesi ilikuwa kubwa sana na ilitawala hisia za watu wengi hasa wananchi wa pande zote mbili ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu nje ya TFF kujua uamuzi wa kamati, na mimi nilijulikana naipenda Yanga aisee nilipata simu nyingi kutoka kila kona sehemu nyingine siwezi kuzitaja,” anasema.
“Nawashukuru sana viongozi wa TFF hasa Rais Wallace Karia katika ile kesi wala hakuwa na sauti yoyote. Nakumbuka aliniambia mwenyekiti nakuachia wewe, ndio maana nimekuamini na kukupata hiyo kamati, simama kwenye sheria mwenye haki iende kwake.
“Halikuwa shauri dogo lile na ndio maana hata sisi tuliamua kufungiana wenyewe, nakumbuka nilimtoa nje Hayati Zacharia Hanspope alikuwa anakuwa mkali tu bila sababu, nikamtimua kwenye kikao akakataa, nikamshtaki kwa Karia akaniambia nawaachia wenyewe mfanye uamuzi, siwezi kumsifia Karia ila penye sifa mpeni.”
Mwanjala anasema na kubainisha kwamba uamuzi wa kamati yake uliwaudhi na kuwafurahisha watu na hakukuwa na jinsi.
BM3 AMHAMISHA NYUMBA
Kiongozi huyo anasema kesi ile ilikuwa ngumu kwani ilisababisha hata kubadilisha magari kila siku kutokana na hisia za wengi akiamua kujilinda ili kuimaliza salama, huku akimtanguliza Mungu kumuongoza.
“Baada ya matokeo ya sakata hilo imewafanya hadi Yanga wenzangu wanichukie na kuonekana adui kwao, lakini ile kesi ilikuwa ngumu na baada ya kesi niliondoka zangu kwenda kwetu Kyela. Baada ya siku moja kulala hotelini niliona isiwe tabu niondoke zangu na uzuri watu wengi walikuwa hawapajui kwangu,” anasema Mwanjala.
“Nashukuru sana Mungu kesi ilipoenda CAS majibu yalikuja na kunipa heshima mimi na kamati yangu, sitaki kuiongelea sana kesi hiyo kwani naweza kuleta vurugu nyingine. Lakini likae vichwani mwa watu kesi ilikuwa na presha ila nilisimamia misingi, haki na taratibu.” Mwanjala anawataka viongozi wa kamati hiyo kuacha mahaba na kufanya kazi kwa haki.
Anasema sakata hilo lilimfanya akae nje ya Dar es Salaam mwezi mzima ili kupisha upepo wa kesi hiyo ambayo ilizua gumzo nchi nzima na hata alipokuwa kwao akitokea mgeni ambaye hakumuelewa, aliamua kujificha.
KUWANIA UONGOZI YANGA
Mwanjala ambaye aliwahi kuongoza Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya kwa miaka minane anasema japo baadhi ya Wanayanga wana makasiriko juu yake akiamua kuwania nafasi ndani ya klabu hiyo anaweza kufanya hivyo, kwani mpira ni sehemu ya maisha yake lakini hofu ni kura nyingi za hapana atakazopigiwa.
“Niliwahi kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti Yanga wakati Mshindo Msolla anagombea. Nakumbuka hata sikuwepo nchini nilikuwa Malawi nilipigiwa simu na Wanayanga nije kugombea. Niliamua kuacha baada ya Rais Karia kuniambia ananihitaji zaidi TFF, nikaona niache,” anasema.
Anasema hata akishindwa kuwa kiongozi ndani ya Yanga hatajutia uamuzi wa kamati yake juu ya sakala la Morrison kwa kuwa alitenda haki na hata akishindwa kuiongoza Yanga atakwenda timu nyingine, lakini sio Simba.
MORRISON KUREJEA YANGA
Anasema mchezaji yeyote mpira ni kazi yake, hata akitokea akarejea Yanga ni sehemu ya maisha yake hivyo hawezi kuchukizwa na hatua hiyo.
“Mchezaji anaangalia wapi pana unafuu wa maisha. Kwa kuwa Yanga sasa hivi wanaonekana wamejijenga hata wachezaji ambao waliondoka wanatamani kurudi tena, kitendo cha kusema anang’ang’anie Simba sio mpango, yeye anaamua nini cha kufanya,” anasema Mwanjala
AJIVUNIA HAYA
Mwanjala anasema katika utawala wake akiwa mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya alipambana kwa kushirikiana na wenzake kuhakikisha kunakuwa na timu za Ligi Kuu.
“Wakati naingia kulikuwa hakuna timu hata moja. Tukajikusanya watu wa Mbeya ambao tulikuwa tunaishi Dar es Salaam na kuamua kuwa kitu kimoja ili kuziinua timu za Mbeya kufika hatua za juu. Nakumbuka nilikuwa mimi, Karua, Seleman Haroub na wengine wengi tu,” anasema.
“Tulianza na malengo zipande Prisons au Mbeya City, lakini tulifanikiwa kuanza na Prisons na kuipandisha ndio ilitufanya kupata CV za kugombea na kuwa viongozi wa mkoa huo. Baada ya kuipandisha tukahamia Mbeya City na tulifanikiwa, tukawa na timu mbili sasa.”
Anasema walipambana kuhakikisha timu ya Kimondo nayo inapanda Ligi Darala la Pili, lakini baada ya Mkoa wa Mbeya kugawanyika hawakuwa na mamlaka nayo kwa kuwa ilihamia sehemu nyingine, ila hawakuishia hapo waliipandisha Boma hadi ikafikia Daraja la Kwanza sasa Championship.
“Hatukuishia hapo katika utawala wangu tukaifufua Tukuyu Stars ambayo ilikuwa imepotea kabisa ikafikia Daraja la Pili na baada ya ajali niliyokumbana nayo kwenye soka, timu nyingi zimeshuka madaraja huko. Kuna timu inaitwa Cocacola ilikuwa inamilikiwa na kampuni ya Coca baadaye ikatwaliwa ikaitwa Mbeya Kwanza nayo imezaliwa kwenye uongozi wangu,” anasema na kuongeza kuwa hata Ihefu walichangia ilipo kwa sasa.
CHANGAMOTO KIBAO
Mwanjala anasema zipo changamoto nyingi katika mpira akiamini kwenye maisha yake kila penye mafanikio hapawezi kukosa maneno mengi kwa kuwa kila mtu ana maono yake.
“Ushirika katika sehemu ya watu wengi ni kazi sana maana wakati wengine mnapambana kuifanya timu ifikie huku, wengine wanapigana iwe hivi wakifurahi kuona mnakwama. Na pia suala la pesa wafadhili ni kazi sana nakumbuka wakati Uwanja wa Sokoine ulipofungiwa tulipata tabu kidogo na wakati huo hatukuwa na pesa na ilikuwa ni lazima tucheze mpira,” anasema.
“Nililazimika kwenda sehemu mbalimbali kununua nyasi kwa wananchi na kuzipanda ili uwanja uweze kurejea. Ndani ya wiki tatu tulipambana hasa. Kitu kingine ni maboresho ya sehemu za kubadilishia nguo nilitumia pesa zangu wakati huo rais alikuwa Jamal Malinzi akatuambiwa atatuletea timu ya Taifa iweke kambi na kweli aliileta Tukuyu.
“Alipokuja kuangalia uwanja akasema hawezi kuleta mechi ya kirafiki ya kimataifa kutokana uwanja ulivyokuwa. Kwa kuwa tunapenda mpira ilitufanya kutumia pesa zetu kuweka ‘tiles’ vyumba vya kubadilishia nguo na vitu vingi zaidi ambavyo vilitumia zaidi ya Sh20 milioni. Nakumbuka Hayati Abbas Kandoro (mkuu wa mkoa wa zamani Mbeya) alitusaidia na halmashauri (ya Jiji la Mbeya) walisaidia milioni mbili mbili na mwisho wa siku mechi haikuchezwa hata kidogo, niliumia sana.”
AZIPA TANO SIMBA, YANGA
Kiongozi wa zamani wa soka anasema haiepukiki nchini mtu wa mpira asipokuwa Yanga, basi atakuwa Simba jambo ambalo liko wazi, akikiri kuwa vigogo wakiamua kumtaka mchezaji fulani hakuna ugumu kumpata kutokana na namna ambavyo wamejijenga.
“Hakuna kiongozi yeyote wa mpira ambaye hana Usimba au Uyanga, vinginevyo kama alikuwa mcheza netiboli, lakini ukiwa kiongozi unatakiwa kusimamia misingi. Hawa Simba na Yanga kwa gharama zao ndio wanabomoa timu, lakini ni umasikini wetu ndio unafanya hivyo,” anasema Mwanjala.
Anatoa mfano Azam FC ina kila kitu ambacho kingeifanya kuwa mbali kwa sasa katika ramani ya soka, lakini imekuwa ngumu kutokana na kumkosa mchezaji wa 12 ambaye anasimama kama ilivyokuwa kwa Simba na Yanga.
“Mchezaji unaweza ukamwambia njoo Yanga nakupa mshahara wa Sh5 milioni au nenda Azam nakupa Sh3.5 milioni hataweza kwenda huko hata kama maslahi makubwa, atakuja Yanga kwa sababu anaweza kupiga simu kwa watu tofauti anaomba 20,000 au 30,000 anapata. Akiwapigia watu 10 kwa siku ana pesa nzuri sana sasa huko Azam anaipataje.”
SAKATA LA MBEYA CITY
Msimu uliopita Mbeya City iliponea tundu la sindano kurejea Champioship ikilazimika kucheza mtoano na Geita Gold na kufanikiwa kubaki kwenye ligi.
“Nakumbuka hiyo mechi ilikuwa ngumu na yenye upinzani mkubwa. Kulikuwa na maneno mengi kwa sababu Geita Gold ndio walikuwa wakitakiwa zaidi na mwenye nchi. Sisi tukawa hivyo tu, nilikuwa na mtihani mkubwa kwa kofia mbili nilizokuwa nazo ya mjumbe wa Kamati ya Utendaji pamoja na mwenyekiti wa Sheria na Hadhi za Wachezaji na huko Mbeya,” anasema.
Anasema wakiwa Sumbawanga kwenye FA alikuwa akimtania Rais Karia anamwambia timu yake ya mkoa itabakia Ligi Kuu na Geita Gold watarejea walikotoka, na ikawa hivyo.
NYAMLANI ALIMPELEKA TFF
Mwanjala anasema hakuibuka tu kama uyoga kuwania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji TFF, bali ni kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo kwenye mpira wa miguu huku Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlan akiwa chachu ya yeye kuwania nafasi hiyo.
“Nyamlani nimesoma naye. Tumetoka mbali sana. Nilipopata uenyekiti Mbeya nikasema ni wakati wetu Mbeya kuwa na uwakilishi ndani ya TFF. Nakumbuka mara ya kwanza nilipingwa na Ayoub Nyenzi kwa sababu wakati ule kulikuwepo na makundi yeye alikuwa upande wa Malinzi na mimi upande wa Nyamlani, basi wale wa upande wa pili walipita wote.
“Mara ya pili nikapambana tena na Nyenzi, lakini wakati ule kanda zikawa zimebadilishwa nikajaribu tena nikafanikiwa kupata kura nyingi,” anasema Mwanjala.
AWAPA SOMO WACHEZAJI
Wachezaji wengi wamekuwa wakikosa haki za msingi katika timu kutokana na aina ya mikataba wanayoingia bila kuwa na tafsiri nzuri kutoka kwa wanasheria wanaozijua vyema sheria.
“Wawe na watu wao wa kuwasimamia, wasiende kichwa kichwa. Kuna vitu vingi nimeviona mle ndani kwao wachezaji siwezi kuvisema hapa. Wengi hawana elimu ya kutumikia mpira hata ukimwambia kitu fanya hivi hakuelewi. Ni wachache sana ambao wana wanasheria wao,” anasema Mwanjala.
Anasema umuhimu wa kuwa na mwanasheria unamfanya hata mchezaji kuwa huru na kufanya kazi moja uwanjani huku mambo mengine yakifanywa na mwanasheria wake.
KIFUNGO CHAKE
Mwaka 2020 alipojitosa tena kuwania nafasi hiyo kuwa watu waliandika barua kuwa amevunja Katiba kwa kugombea mara tatu badala ya mbili, ndipo ulipokuwa mwisho wake baada ya kufungiwa miaka miwili kwa kosa la kukiuka Katiba ya chama cha soka mkoa.
“Hiyo Katiba wakati nimeingia madarakani sikuiona na niliyotumia ilikuwa ni ya mwaka 2004 inayoruhusu vipindi vitatu. Kumbe watu katiba walikuwa nazo wamezificha zikisema miaka miwili sasa sikujua ni kwa sababu gani walifanya hivyo na hadi sasa mimi sio kiongozi wa mpira maana nilipigwa pini Desemba mwaka juzi,” anasema.
Anasema uchaguzi unasimamiwa na TFF, lakini anashangaa hadi wanaruhusu unafanywe na baadae wanaona kulikuwa na upungufu na kuadhibiwa huo upungufu hata yeye alishindwa kuelewa, lakini mwisho wa siku aliamua kumwachia Mungu japokuwa ni uamuzi uliomuumiza.
Mwanjala anasisitiza kuwa mpira ni ugonjwa mwilini mwake na maisha yake, hivyo hawezi kusema kama kifungo hicho kimemtoa kwenye reli au ataendelea na uongozi kwa mara nyingine, kwani ni miezi sita imesalia adhabu yake imalizike.
“Kifungo hicho kilitokea kutokana na ujinga wangu mwenyewe, lakini wanisamahe, basi hata kidogokidogo japokuwa siwezi kusema ni kifungo kikubwa au vipi.”
KARIA MWAMBA
Mwanjala anasema kila uongozi unakuwa na bahati, lakini Karia katika hilo amefaulu na yeye kama mdau wa soka anampongeza na watendaji wenzake kwa hatua ambazo timu za Taifa zimefikia kwa sasa.
“Toka Uhuru na kabla ya Uhuru, Karia amekuwa na bahati sana katika utawala wake. Tumecheza Chan, Afcon, timu ya wanawake inaenda Kombe la Dunia, naona ni mtu ambaye anastahili kupewa muda zaidi maana kila uongozi una bahati,” anasema.
“Kuna kiongozi wetu mmoja hapa alikuwa mzuri sana, lakini hakuwa na bahati mfano Leodegar Tenga alikuja kujenga utawala bora maana zamani TFF ilikuwa kama genge, akajitahidi kuibadilisha ikawa taasisi inayoeleweka sasa Karia akasema Tenga kafanya hivi na mimi naenda kucheza mpira na kweli tunaona mabadiliko.”
MFUMO UWEKEZAJI SIMBA, YANGA
Mwanjala anasema ni hatua nzuri ambazo timu hizo zinapitia kwa sasa kwa kuwa soka la kisasa ni pesa duniani kote.
“Tatizo la timu zetu mbili hizi Simba na Yanga anaweza akaja mwanachama mmoja akaibuka na jambo mambo yakavurugika. Wajitahidi kuufahamu mfumo ili mambo yaende sawa. Napenda sana mabadiliko haya ila wanachama waepuke migogoro,” anasisitiza huku akiunga mkono hoja ya mwekezaji zaidi ya mmoja katika mifumo hiyo.
AIPA TANO SIMBA, YANGA IIGE
Anasema baadhi ya watu wanaona Simba imezorota jambo ambalo si kweli kwa kuwa hatua ya kuingia robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika si mchezo.
“Simba wamefanya vizuri sana. Hata hao Yanga na wao wasione tabu kuiga alichoanya Simba hadi kufikia hatua aliyoifikia, wajitahidi kubadilika hasa pale timu za nje zinapokuja kucheza Tanzania waungane na kusapotiana, lakini utani wa jadi uendelee,” anasema.
VIWANJA
Mwanjala anasema suala la viwanja nchini ni zaidi ya changamoto, lakini akazipongeza timu kama Azam FC, Gwambina, Ihefu na nyingine zilizofanikiwa kuwa na viwanja vizuri vinavyozidi kuongeza chachu kwa wachezaji na hata timu nyingine. “Ukiwa na uwanja utacheza mpira. Ni shida kubwa hapa nchini, maana Fifa hawawezi kuwekeza kwenye viwanja vya siasa, vya Serikali, wanaweza na ndio maana Kaitaba wamewekeza ila huku kwingine ni shida, mfano uwanja wa Sumbawanga, Kigoma imepelekwa fainali ya FA sasa huko hakuna timu viwanja vinazidi kuharibika,” anasema.
“Simba na Yanga na ukongwe wa miaka walionayo walistahili kuwa na viwanja vyao na sio wa Taifa (Mkapa) wanaoutumia ila siasa za mpira ndizo zimewafanya wawe hapa walipo hivi sasa. Lakini wakimaliza mambo yao ya uwekezaji wataweza kuwa navyo viwanja.”
MWANJALA NI NANI
Alianza kuongoza mpira Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (TEFA) akiwa mjumbe wa soka la wanawake. Baada ya hapo akaamua kujitosa kugombea uenyekiti wa Chama cah Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa).
Mwaka 2010 alijitosa kuwania nafasi hiyo ambayo aliitumikia kwa weledi na kujitolea mambo mbalimbali ikiwemo fedha zake za mfukoni.