Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Muhene ‘Try Again’ amehudhuria kozi ya Diploma in Club Management) inayotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) inayofanyika Sydney, Australia.
Try Again amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Rais wa FIFA, Gianni Infantino kuhusu michuano ya Africa Super League ambayo Simba itashiriki pamoja na maendeleo ya soka nchini Tanzania.
"Nimefurahi kukutana na Rais wa FIFA, Infantino pamoja na mkurugenzi wa maendeleo ya mpira wa miguu Ornella Desiree Bellia kujadili kuhusu Super League. Majadiliano yamekuwa mazuri na jambo jema Rais Infantino anaielewa vizuri Tanzania.
"Ameahidi atakuwepo kwenye uzinduzi wa Super League ambao utafanyika Tanzania. Tupo hapa Sydney kushiriki kozi ya Diploma katika uongozi wa klabu inayotolewa na FIFA lakini pia kufanya shughuli za mpira ikiwepo pia kujifunza namna mashindano makubwa yanavyoandaliwa kama Kombe la Dunia la Wanawake ambalo linafanyika hapa Australia na Newzealand.
"Kama mnavyofahamu Simba itashiriki katika Africa Super League hivyo uzoefu huu utatusaidia katika uandaaji wa sherehe za ufunguzi pamoja na michezo ya Kimataifa iliyopo mbele yetu," alisema Try Again.