Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigogo Bayern aichimba mkwara Real Madrid

Image 149 1140x640.png Kigogo Bayern aichimba mkwara Real Madrid

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: Dar24

Rais wa klabu Bingwa nchini Ujerumani FC Bayern Munich, Herbert Hainer ameifahamisha Real Madrid hawana mpango wa kumuuza Aphonso Davies mwishoni mwa msimu huu.

Imeripotiwa Real Madrid ina nia ya kumsajili beki huyo kutoka nchini Canada kwenye usajili wa kiangazi lakini bosi huyo ametoa tahadhari kwa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Mabingwa Ulaya.

Madrid wameongeza kasi ya kunasa saini ya Davies katika miezi ya hivi karibuni na inaripotiwa inafikiria kufikia bei ya Pauni 34 milioni kwa ajili ya beki huyo wa kushoto.

Hata hivyo, miamba ya Bundesliga wanasita kumuuza mmoja wa wachezaji wao muhimu kwani beki huyo wa kimataifa wa Canada amekuwa na mchango mkubwa.

Kocha wa Madrid, Carlo Ancelotti anatazamia kuimarisha nafasi ya beki wa kushoto huku Ferland Mendy akipambana kuwa fiti msimu huu kwani anasumbuliwa na majeraha.

Davies anatajwa kuwa usajili namba moja ambao umetolewa macho na Los Blancos miezi ya hivi karibuni, huku wakala wa mchezaji huyo akikiri mteja wake atakuwa tayari kuhama Ujerumani kabla ya mkataba wake kumalizika mwaka 2025.

Lakini Bayer imepuuza tetesi hizo na Rais Herbert Hainer akisema: “Davies yupo na sisi hadi mwaka 2025, ni mmoja wa mabeki bora zaidi duniani. Bila shaka tunataka abaki na natumaini hata yeye hana mpango wa kuondoka.”

Davies amekuwa mchezaji muhimu kwa The Bavarians mwaka huu, akianza michezo 10 kati ya 11 ya Bundesliga na kutoa pasi tatu za mabao kwa upande wa Thomas Tuchel.

Chanzo: Dar24