Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kifukwe arejeshewa ubosi Tanzania prisons!

Kifukwe Pic Kifukwe arejeshewa ubosi Tanzania prisons!

Fri, 16 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Tanzania Prisons wamemrejesha, Ajabu Kifukwe ndani ya uongozi wa timu hiyo akiwa katibu akichukua nafasi ya Anthony Hau ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Kifukwe alikuwa kwenye nafasi hiyo lakini misimu miwili iliyopita alipangiwa kazi nyingine lakini kwa sasa amerejea na kazi kubwa ni kuhakikisha Tanzania Prisons inarejesha makali yake kwa sababu msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja baada ya kujinasua kwenye michezo ya hatua ya mtoano.

Kifukwe alisema anachotaka ni ushirikiano na viongozi wenzake, benchi la ufundi pamoja na wachezaji ili kuifanya Prisons kuwa imara kila wakati hasa kwa michezo ya lala salama ya Ligi Kuu na michuano mbalimbali ikiwemo Kombe la Azam (ASFC) ambayo tayari imetinga hatua ya 32 baada ya kuichapa Misitu FC mabao 7-1.

“Hapa ni nyumbani sina jambo jipya zaidi ya kufanya kile ambacho wenzangu walikuwa wanakifanya nami nitaendeleza kwa kushirikiana nao na yale ambayo niliacha wakati naondoka ambayo hayakufanyika na bado yana umuhimu, basi nitayafanya kwa faida ya timu yetu.

“Tayari nimepokea ripoti ya kocha kuhusu dirisha dogo la usajili na mambo mengine, lakini haya yote tunatakiwa kuyafanya kwa uangalifu ili kukimbizana na muda na kuifanya timu kuwa pamoja kwa muda wote ambao Ligi Kuu inaendelea,” alisema Kifukwe.

Kwa upande wa Hau aliushukuru uongozi kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuongoza kwa muda aliokuwa madarakani na sasa akimpisha Kifukwe na kumuahidi kumpa ushirikiano.

Jumamosi hii Tanzania Prisons itakuwa nyumbani katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuikaribisha Singida Big Stars huku ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja Liti, Singida kwa bao 1-0 lililofungwa na Peterson Cruz dakika ya 36.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Shabaan Mtupa alisema timu ipo vizuri kwa ajili ya mzunguko wa pili baada ya kumalizika nafasi ya 11 na alama 15 sawa na Coastal Union ambayo ipo nafasi ya 12 baada ya mapumzuko ya wiki moja kupisha ASFC na imejiimarisha zaidi kwa michezo ya lala salama.

Chanzo: Mwanaspoti