Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kifo cha Raiola kilivyompa Rafaela uwakala kwa Haaland

Haaland Uwakalaaaa Kifo cha Raiola kilivyompa Rafaela uwakala kwa Haaland

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Aprili 1, 20, 2022, dunia ilimpoteza mmoja kati ya mawakala wakubwa wa soka, Mino Raiola. Ilikuwa ni siku mbaya kwa wachezaji wakubwa kama Erling Haaland, Paul Pogba na Gianluigi Donnarumma, mzee huyu alikuwa ni kama baba kwao kwa sababu aliwalea kimpira tangu wakiwa na umri mdogo hadi kufanikiwa kuwa wachezaji wakubwa.

Alisifika kwa jicho lake la kutazama wachezaji wakiwa na umri mdogo kisha kuwatengenezea njia na baadaye wakaja kufanikiwa.

Raiola aliacha zaidi ya wachezaji 50 waliokuwa chini yake. Baada ya kufariki kwake swali kubwa lilikuwa ni nani atawasimamia wachezaji hao ambao kwa sasa ndio wapo kwenye nyakati zao bora kama vile Erling Haaland.

Kwenye ofisi ya Raiola kule nchini Italia, kulikuwa na mama mmoja aliyehudumu kama mwanasheria.

Rafaela Vitale Pimenta alikuwa na kazi ya kuhakikisha anapitia mikataba yote ya wachezaji na kuidhinisha. Pia alilazimika kufuatilia kesi mbalimbali za wachezaji walio chini ya Raiola ikiwa zile za madai na masuala mengine ya kisheria.

Haikuwahi kutazamiwa kwamba siku moja anaweza kuwa wakala wa mastaa wakubwa kama hawa alionao kwa sasa.

Ilikuwa miaka ya 2000, pale Pimenta alipokutana na Raiola huko Brazil kwenye mechi ya hisani iliyoandaliwa na wachezaji wa zamani wa Brazil, Rivaldo na Cesar Sampaio.

Baada ya kukutana hapo wakati huo, Pimenta akiwa ametoka kuacha kazi ya serikali ambako alikuwa akihudumu kama mwanasheria, Raiola alimpa ofa ya kwenda kuwa mwanasheria wa wachezaji wake. Pimenta akakubali.

Alikuwa mkono wa kulia wa Raiola na mara zote wakala huyo alipokuwa akienda kumaliza madili basi Pimenta alionekana.

Licha ya ukaribu wao haikuwahi kutazamiwa kwamba siku moja mama huyu angechukuwa nafasi ya Raiola kwa kurithi wachezaji, kwani iliaminika labda Raiola angewarithisha wachezaji kwa watoto wake.

Haikuwa hivyo, moja ya maelekezo ambayo, wakala huyu aliyatoa kabla ya kufariki ni wachezaji wote kuwa chini ya uangalizi wa Pimenta.

Ghafla tu, kibarua anakuwa bosi. Ghafla akajikuta amekuwa wakala wa kundi kubwa la wachezaji wanaoisumbua dunia.

Mwenyewe mara kadhaa amewahi kunukuliwa akisema kwamba kibarua hicho kimekuwa kigumu sana kwa sababu mawakala wengi wanawatamani wachezaji ambao yeye anawamiliki.

Ndio, nani asingetamani kuwa wakala wa mchezaji kama Erling Haaland, nani asingetamani kuwa wakala wa Gianluigi Donnarumma, Marco Verratti, Matthijs de Ligt, Xavi Simons, na Gravenberch, lakini wote hao wamerithishwa kwa Pimenta anayeonekana kuamka akiwa na kuamka tajiri.

Kawaida kwenye kila uhamisho wa wachezaji huwa kuna ada ya uwakala ambayo ni pesa anayoipata wakala. Kiasi hicho huwa ni asilimia 10 ya pesa ya usajili. Sasa ili wakala apate pesa nyingi lazima mchezaji wake anunuliwe ama aongeze mkataba kwa pesa nyingi pia. Hivyo Pimenta atapata pesa za kutosha kwa sababu wachezaji wengi walio chini yake kwa sasa wapo kwenye nyakati zao bora na wanaendelea kuonyesha kiwango bora kiasi cha kila timu kutamani kuwa nao.

Chanzo: Mwanaspoti