Msemaji wa Klabu ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema utabiri wake wa kuipa Ubingwa Young Africans msimu huu umetimia, na hana deni kwa mashabiki wa Soka ambao walikua wakihoji kwa nini alitabiri hivyo mwanzoni mwa msimu huu.
Kifaru amesema utabiri wake wa kuipa Ubingwa Young Africans mwanzoni mwa msimu huu, ulitokana na kuisoma timu hiyo ya Jaangwani namna ilivyokua ikicheza, ikiwa na wachezaji wenye uwezo wa kupambana hadi mwishoni mwa msimu huu.
“Niliitabiria Ubingwa Young Africans mapema sana kama watachukua ubingwa, ninaamini watu wameamini nini nilikua namaanisha kipindi kile, nakumbuka ilikua baada ya mchezo wa kwanza ama wapili kwa msimu huu, na sasa yametimia,”
“Niliona namna walivyosajili na walivyocheza mwanzoni mwa msimu, nikajiridhisha kuwa hawa jamaa kuna jambo wanalihitaji msimu huu, imekua hivyo, kwa hiyo sina deni na utabiri wangu, pia nimewajibu wale walioshtushwa na nilichokitabiri mwanzoni mwa msimu.” Amesema Kifaru
Kuhusu Simba SC Kifaru amesema: “Simba haikuwa na nafasi ya kuchukua ubingwa msimu huu, ilianza vibaya na wachezaji wake wameonyesha kuzinduka katika michezo ya mwisho, kweli Simba wana timu nzuri lakini msimu huu kuna kitu walikikosea,”
“Unapoanza msimu kwa kusuasua ni bahati sana kumaliza ukiwa na mafanikio makubwa, wenzao Young Africans walianza kwa kasi kubwa na ndio maana imewalazimu kumaliza kwa kasi ile ile na wametwaa Ubingwa.”
Young Africans itakabidhiwa Kombe la Ubingwa mwishoni mwa juma hili jijini Mbeya baada ya mchezo wake na Mbeya City FC itakayokuwa nyumbani Uwanja wa Sokoine.
Kwa sasa Young Africans iliyocheza michezo 28 imejikusanyia alama 70, ikiwa na michezo miwili mkononi, huku wapinzani wao Simba SC wakiwa nafasi ya pili baada ya kucheza michezo 28, wakikusanya alama 60.