Simba imefanya maamuzi magumu ya kumpiga chini kipa Mbrazili Jefferson Luis aliyesajiliwa hivi karibuni kwa madai ya kuwa amepata majeraha makubwa, hivyo amesitishiwa mkataba kwani atakuwa nje kwa muda mrefu.
Chanzo chetu cha kuaminika kinasema kwamba Jefferson alisajiliwa huku akiwa na tatizo la misuli nyuma ya paja lililogundulika juzi mazoezini, huku jina lake likiwa tayari katika usajili wa CAF.
“Ni kweli amegundulika na tatizo hilo, anaweza kukaa nje kwa muda mrefu ila siwezi kusema moja kwa moja kama mkataba utavunjwa au lah! Maana maamuzi hayajafikiwa,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.
Akizungumzia sakata hilo, mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Amri Kiemba amesema kuwa majeraha ni kawaida kwa mchezaji hivyo sio jambo la mahasimu wao kuwacheka Simba kwamba wamepigwa au wameuziwa mchezaji mbovu.
"Kuumia kwa wachezaji ni matukio ya kawaida ndio maana kuna wachezaji wanaumia hata kwenye warm up na kulamisha mpango kazi wa mwalimu ubadilike kwa hiyo kama kipa wa Simba kaumia na dirisha la usajili bado lipo wazi wanaweza kutafuta mbadala.
"Bahati nzuri kwa Simba wataanzia hatua ya pili kwenye mashindano ya kimataifa kwa hiyo watakwenda hadi mwishoni mwa mwezi Agosti, bado wana muda wa kutosha kulifanyia kazi hilo na kupata golikipa.
"Wakati wanansajili Jefferson Luis bila shaka kitengo cha scouting kilikuwa na majina kadhaa ila Luis ndio akachukuliwa, watudi kwenye ma-file waangalie waliobaki wachukue mwingine," amesema Amri Kiemba.
Kwa upande wake, Ofisa Habari Simba SC, Ahmed Ally amesema ripoti ya daktari itakayotolewa juu ya kipa wao Luis aliyeumia mazoezini nchini Uturuki ndiyo itakayoamua juu mustakabali wake kwenye klabu hiyo. Amedai ikiwa majeraha yatamweka nje kwa muda mrefu, watamuacha," amesema Ahmed.