Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kichuya ampigia debe Morrison kutua Jeshini

Morrison Ds Bernard Morrison

Thu, 13 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Winga wa JKT Tanzania, Shiza Kichuya, ameweka wazi kutamani kucheza na Bernard Morrison katika kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo JKT Tanzania na timu nyingine zinazomilikiwa na majeshi, hazina ruhusa ya kusajili wageni kwa sasa mpaka pale sheria zitakapobadilishwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kichuya, alisema angependa kuona nyota huyo raia wa Ghana anasajiliwa katika timu hiyo kutokana na uwezo aliokuwa nao na anaamini atawasaidia kufanya vyema kwenye msimu mpya.

Kichuya alisema nyota huyo wa zamani wa Simba na Yanga anaijua vyema Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo uwepo wake utaongeza ubora wa timu yao.

"Akisajiliwa JKT Tanzania nitafurahi sana kwa sababu ni mchezaji mkubwa, ana uzoefu, ni mchezaji wa kimataifa, ana vitu vingi, ana kipaji kikubwa, anajua muda huu nini timu inatakiwa kufanya, na wakati wa kuibeba timu mgongoni mwake kwa kutumia uwezo na kipaji alichonacho, nadhani kila mtu anafahamu ni vitu gani alikuwa anavifanya akiwa Simba na Yanga," alisema Kichuya.

Morrison alionekana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, unaomilikiwa na Maafande hao katika mchezo wa 'play off', kati ya JKT Tanzania dhidi ya Tabora United uliomalizika kwa suluhu.

Baada ya mechi hiyo kumalizika, Kichuya na Said Ndemla, ambao waliwahi kuichezea Simba, walionekana kufurahi kumwona Morrison na kuzungumza kwa muda mrefu.

Kwa sasa Morrison ni mchezaji wa FAR Rabat ya Morocco, lakini inadaiwa yuko nchini kwa ajili ya kupata matibabu baada ya kuumia akiwa na timu hiyo.

Mbali na nyota huyo, wachezaji wengine wa kigeni waliowahi kuzitumikia Simba, Yanga na Azam wapo nchini kwa kile kinachoelezwa kusaka timu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live