Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kichuya, Kabunda wategwa Namungo

Kichuya Qs Vita Kichuya, Kabunda wategwa Namungo

Wed, 27 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Namungo imecheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara bila kuonja ushindi wowote huku ikifunga bao moja tu, kitu kilichomshtua kocha mkuu wa timu hiyo, Cedric Kaze na kuamua kukaa na wachezaji akiipa kazi safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kuhakikisha inarejesha makali ya kutupia nyavuni ili timu itoke eneo la chini.

Namungo imetoka kupokea kipigo cha 1-0 kutoka kwa Yanga katika mechi iliyotumia mbinu ya kupaki basi, huku katika mechi mbili za awali ikipoteza kwa JKT Tanzania na kutoka sare ya 1-1 na KMC, mechi pekee iliyopata bao lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Mkongomani, Fabrice Ngoy wa Ngoy, lakini kocha Kaze amesema wamerejea mazoezini huku kazi kubwa ikiwa ni kushughulikia eneo la ushambuliaji.

Akizungumza nasi, Kaze alisema licha ya eneo la ulinzi kuruhusu mabao lakini angalau kumekuwa na maelewano mazuri kwenye uchezaji tofauti na ushambuliaji ambako bado hakujatulia.

“Ni kweli tumeruhusu mabao mengi hadi sasa lakini ukiangalia pia nafasi tunazopoteza ni nyingi jambo ambalo sio mwanzo mzuri kwetu hivyo tunaendelea kulifanyia kazi,” alisema Kaze na kuongeza;

“Tuna washambuliaji wazuri ila changamoto imetokea baada ya kupata majeraha lakini tuna imani hadi kufikia mchezo wetu ujao, basi tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuwaona wakirudi uwanjani.”

Timu hiyo ina washambuliaji hatari kama Reliants Lusajo, Hassan Kabunda, Pius Buswita, Ibrahim Mkoko, Shiza Kichuya, Kelvin Sabato ‘Kiduku’, Ngoy na wengine, ambao kwa mazoezi na vikao walivyofanya na Kaze watakuwa na kazi ya kuibeba timu hiyo inayoshika nafasi ya 14 kwa sasa ikiwa na pointi moja tu.

Kwa sasa Namungo inajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa utakaopigwa Septemba 30 kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi ukiwa ni wa tatu nyumbani baada ya ule wa KMC na JKT.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live