Kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kuwa amefurahishwa na kiwango kilicho onyeshwa na wachezaji wake katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers.
Robertinho amedai pia kukoshwa na namna walivyocheza kitimu hasa kipindi cha pili huku muunganiko wa wachezaji vijana na wazoefu ukiwa mzuri.
“Katika Ligi ya Mabingwa hasa hatua ya makundi ushindi ndilo jambo linalotakiwa, iwe moja, mbili au nne kinachoangaliwa ni pointi tatu.
"Tumecheza vizuri, tulikuwa na muunganiko mzuri mbinu yetu ilikuwa kuhakikisha tunapata ushindi, kipindi cha pili muunganiko wetu uliimarika, kasi iliongezeka iliyochangiwa na wachezaji vijana na wazoefu,” amesema Robertinho.
Mbrazil huyo ambaye alikuwa ameshaanza kurushiwa maneno na baadhi ya mashabiki wa Simba wakishinikiza avunjiwe mkataba kwa matokeo mabovudhidi ya Raja na Horoya, hakusita kuwasifia Vipers kwa mchezo waliyocheza na kuwapatia upinzani mkubwa muda wote wa mchezo.