Klabu ya Simba imehitimisha mchezo wa hatua ya makundi, Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kupoteza bao 3-1 dhidi ya wenyeji Raja Casablanca mtanange uliopigwa dimba la Mfalme Mohamed V Jijini Casablanca, Morocco.
Kwenye mchezo ambao timu zote mbili zilikuwa zimefuzu kuingia robo fainali, Simba walionekana kucheza vizuri karibu dakika 40 za mchezo kabla ya kuruhusu bao la kwanza dakika za mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa Hamza Khabba akitumia pasi ya kichwa ya Yousri Bouzok.
Kipindi cha pili yakafungwa magoli matatu, mawili kwa Raja kisha moja kwa upande wa Simba.
Khabba akafunga bao la penati kufuatia makosa ya Joash Onyango kisha bao la mwisho likafungwa na Mohamed Boulacsout wakati bao la Wekundu wa Msimbazi Simba likawekwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Congo Jean Baleke akitumia pasi murua ya Mzamiru Yasni.
Bao la Baleke upande wa Simba linakuwa la kwanza kwa Raja Casablanca kufungwa katika uwanja wao wa Mfalme Mohamed V katika hatua ya makundi.
Kwa matokeo hayo, Raja Casablanca inafikisha pointi 16 kileleni mwa Kundi C, ikifuatiwa na Simba yenye pointi tisa na zote zimefuzu Robo Fainali zikiziacha Horoya yenye pointi saba na Vipers pointi mbili zikiishia hatua ya 16 Bora.