Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiburi cha Jangwa feki kilipokwama kwa Jangwa asilia

Yanga Algeria Tiziiiiii Kiburi cha Jangwa feki kilipokwama kwa Jangwa asilia

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga ambao wanaishi eneo linaloitwa Jangwani jijini Dar es Salaam, Ijumaa usiku walikuwa wakicheza kando ya jangwa halisi la Sahara kando ya jiji la Algers. Kiburi chao kilikoma katika jiji hilo baada ya kuanzisha utawala wa muda mfupi katika soka la Afrika.

Baada ya kumchapa mtani wao Simba mabao 5-1 Yanga walikuwa wameendeleza kiburi chao cha kuzifunga timu kubwa au zilizowekeza Afrika. Simba, Azam, TP Mazembe, Monastir, USM Alger na wengjneo kadhaa. Hawakuwafunga kwa bahati mbaya. Wana uwezo kwa sasa.

Ghafla wakakutana na timu inayoitwa CR Belouizdad ya Algeria katika mechi ya kwanza ya kundi lao la Ligi ya Mabingwa Afrika. Pambano lilichezwa ugenini na Yanga waliamua kucheza kama wapo Uwanja wa Taifa. Hiki ni kiburi walichokipata baada ya kuwa fiti na kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo kwa sasa.

Walichapwa mabao 3-0 katika jiji la Algers, huku bao la kwanza likija kutokana na kosa la beki wa kati, Ibrahim Bacca ambaye hafanyi makosa mengi katika mchezo wa soka kwa sasa. Ilikuwa bahati mbaya wakati alipoukosa kizembe mpira wa kona wa wenyeji ambapo badala yake mpira uliangukia kwa mchezaji wa wenyeji aliyefunga bao la kwanza.

Baada ya hapo Yanga wakauchukua mchezo wao. Sidhani kama ulikuwa ni mpango wa Belouizdad kukaa nyuma baada ya kupata bao la kuongoza. Nawajua Waarabu.

Akikufunga anataka kukufunga tena na tena. Ni ubora wa Yanga ndio ambao uliwafanya wakae nyuma ya mpira kwa muda mrefu. Yanga wakatawala soka.

Yanga walionekana wanataka kurudisha bao na kushinda mechi mbele ya mashabiki lukuki wa wenyeji. Aliyekuwa anaongoza jambo lao alikuwa mchezaji anayeitwa Pacome Zouzoua. Jamaa ni bonge la mchezaji. Ana kila kitu ambacho kiungo mshambuliaji anapaswa kuwa nacho. Ana akili ya mpira na ana umiliki mkubwa wa mpira.

Anateleza. Anautaka mpira. Anajaribu kufanya jambo litokee. Anaunganisha timu. Wengine pia walikuwa wanajaribu kuucheza muziki wake, lakini haikuwa siku nzuri kwa Maxi Nzengeli wala Stephane Aziz Ki ambao kwa miezi michache tangu waungane Jangwani wamejaribu kuutengeneza utatu mtakatifu ambao umefanya kazi nzuri Jangwani.

Nyodo za kujaribu kucheza vizuri na kusaka bao la kusawazisha wakiwa ugenini zikawaponza Yanga. Mida fulani ta kipindi cha pili wakaupora mpira ambao uliwaacha washambuliaji wawili wa Belouizdad wakitazamana na beki mmoja wa Yanga, Dickson Job sambamba na kiungo Nzengeli pamoja na kipa wao, Metacha Mnata. Ni moja kati ya kazi ngumu kwa watu wanaopaswa kukabiliana na shambulizi la kushtukiza (counter attack).

Majuzi nilikuwa nawasifu Yanga namna ambavyo wanakuwa bora wakati hawana mpira. Katika mechi hii hawakuwa na ubora wowote ule wakati hawana mpira. Walijisahau na kujiona wao ni Al Ahly. Walijisahau na kujiona wao ni Mamelodi Sundowns. Wakajisahau na kujiona wao ni Man City. Kwamba shambulizi lao linapaswa kuishia katika bao, au kona, au ‘goalkick’.

Hapa Yanga wakafungwa bao la pili kutokana na shambulizi la kushtukiza la wenyeji. Mchezo ukaendelea kwa aina hii hii. Yanga wakawaingiza Yesu wao, Jesus Moloko. Halafu wakamuingiza Clement Mzize. Unaweza kubakiwa na mkanganyiko wa mawazo. Zamani kabla ya mechi, katika mechi ya aina hii sare ingeweza kututosha lakini Ijumaa usiku hali ilikuwa tofauti.

Ijumaa usiku ilikuwa aina ya mechi ambayo Yanga walidhani wangepaswa kusawazisha na kuongeza bao jingine. Wakapoteza nidhamu ya mchezo. Wakaishia kufungwa bao la tatu la kizembe wakati huo wakiamini kwamba wangeweza kuifanya mechi imalizike kwa sare ya 2-2. Mpira wote ulikuwa katika 18 ya wenyeji.

Wazee wa Jangwa asilia wakaupata mpira na kuupeleka katika lango la Yanga. Ilikuwa rahisi kwao kufunga bao la tatu na kweli wakafunga. Hapa ndipo ambapo Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi inabidi afanye kazi zaidi. Haijalishi mechi imesimama wapi lakini wachezaji wanapaswa kukumbuka majukumu yao kwa muda wote.

Niliwapenda Yanga kwa nidhamu ya wakati hawana mpira lakini sio kwa Yanga ya Ijumaa usiku. Hawa walikuwa wamesambaratika. Walikuwa wanajiona wanastahili kusawazisha kuliko kuongezwa bao jingine.

Belouizdad waliwafundisha adabu na wakafanikiwa. Sikumbuki ni lini mara ya mwisho Yanga ya rafiki yangu Injinia Hersi Said ilifungwa mabao matatu, lakini hii ilifungwa bao la tatu mbele ya wote sisi.

Walifungwa bao hili wakiwa na washambuliaji wote uwanjani. Hafiz Konkoni, Mzize na Kennedy Musonda. Wakati mwingine unajiuliza, ni jambo la kujivunia au la kupuuza? Kwamba tumefikia kiburi hiki au sare ya ugenini ingetosha kwa Yanga? Jibu unalo. Binafsi naamini Yanga walipoteza nidhamu ya namna ambavyo michuano hii unapaswa kushiriki.

Sawa, wana timu ya maana. Sawa, walifika katika fainali za michuano ya Shirikisho lakini katika namna hii ya michuano wakati mwingine unahitaji walau sare tu ugenini. Baada ya bao la kwanza la Belouizdad walihitaji sare tu, lakini wakaenda mbali kutamani ushindi. Hapa ndipo walipoadhibiwa.

Kundi lao sio baya lakini kunahitajika umakini wa hali ya juu kuanzia sasa na kuendelea. Mechi ijayo ni dhidi ya Al Ahly pale Temeke. Sikutazama vizuri pambano la Al Ahly dhidi ya Medeama pale Cairo, lakini imeshinda nyumbani kwa mabao 3-0.

Unapojikumbusha kwamba Al Ahly walishinda lakini walipata bao lao la kwanza kuanzia dakika ya 65 na kuendelea hii inakupa tafsiri tofauti. Al Ahly wamepungua kiwango au Medeama wana ubora?

Yanga wamesahau matokeo ya mechi hii na wanatazamiwa kuwakaribisha Al Ahly pale Temeke katika mwanzo mpya wa Desemba. Matazamio makubwa kwa Wanayanga ni kwamba wanaweza kushinda pambano hilo hasa baada ya kutazama mechi mbili za mwisho za watani wao Simba dhidi ya Al Ahly ambazo zote mbili ziliisha kwa sare katika michuano mipya ya African Football League (Super League).

Chochote ambacho kinaweza kutoka kando ya pambano hilo kisiwe kufungwa kinaweza kuwasadia lakini wakifungwa basi watakuwa na mlima mkubwa wa kupanda kuweza kutinga robo fainali yao ya kwanza ya michuano hii tangu mwaka 1998. Zamani sana. Nje ya hapo watakuwa wametanguliza mguu mmoja nje kuelekea katika mlango wa kutokea katika michuano hii.

Baada ya mechi hiyo dhidi ya Al Ahly watabakiwa na mechi mbili ambazo kiratiba zinaonekana rahisi. Dhidi ya Medeama ugenini halafu nyumbani. Wakati huo Al Ahly watakuwa wakihangaishana na Belouizdad nyumbani na ugenini. Kwao itakuwa nafasi ya kujaribu kupata pointi sita huku Al Ahly na Belouizdad wakipunguzana wenyewe kwa wenyewe.

Ni rahisi kupiga hesabu hizi katika vidole lakini sio rahisi kupiga hesabu hizi uwanjani. Yanga wanahitaji nidhamu kubwa ya mchezo uwanjani. Hii sio michuano rahisi sana.

Kwa kuanzia tusubiri kuona mechi mbili zijazo za kundi hili zitakwenda vipi. Kwa sasa tushikilie mioyo yetu tu. Kesho tutamchambua mnyama katika mechi yake ya Jumamosi jioni dhidi ya ASEC Mimosas.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: