Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibu kazidi kuonesha kwa nini wazawa hawaaminiki

Kibu Denis Carlos Kibu kazidi kuonesha kwa nini wazawa hawaaminiki

Mon, 29 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuna wakala mmoja wa wachezaji, aliwahi kuniambia ukimpeleka mchezaji wa Kitanzania nje ya nchi mpaka wamchukue au kumfanyia majaribio ni lazima awe na barua kutoka klabu yake ya mwisho aliyotoka, vinginevyo hawatomruhusu kufanya chochote.

Akasema sababu kubwa klabu nyingi za nje wameshawahi kuingia matatizoni kwa kuwafanyia majaribio wachezaji ambao wana mikataba na klabu wanayotoka. Akasema baadhi ya klabu zimeshawahi kulipa faini kutokana na hilo, kwani wachezaji walikuwa wakizidanganya kuwa hawakuwa na timu, yaani wapo huru.

Na hilo limekuwa likiwafanya wasiaminike tena kwenye klabu na wakati mwingine kutowaongeza mikataba wanapomaliza ile ya kwanza. Sakata la Kibu Denis ambalo limeshika chati kwa kiasi cha wiki nzima kwenye vipindi vya michezo, vijiweni, mitaani na mitandao ya kijamii, limenifanya nimkumbuke wakala huyo.

Sitaki kueleza mengi jinsi alivyokuwa mapumzikoni nchini Marekani, halafu wakati wenzake wanataka kwenda nchini Misri yeye akaenda Kigoma na baada ya hapo akatoweka huku kikosi cha Simba kikiwa kwenye maandalizi ya msimu huko Ismailia, Misri.

Hakuna aliyejua amekwenda wapi, hata wasimamizi wake nao walipoulizwa hawakujua yupo wapi, klabu nayo haijui, hali ambayo ilisababisha mtafaruku mkubwa.

Taarifa zikadai kuwa ametorokea Ulaya kusaka malisho, lakini kila mmoja akashangaa uondokaji wake wakati ana mkataba mbichi na Klabu ya Simba, iliyomsajili kwa mbinde. Baada ya sakata zima, imeelezwa kuwa kumbe alitimkia nchini Norway kwenye Klabu ya Kristiansund BK.

Kwa akili yake alidhani angeweza tu kwenda na kusajili bila klabu yake kufahamu, au kuna kitu alitegemea. Wengi wanaofahamu mpira wa kisasa hasa wa kulipwa unavyoendeshwa, walijua hata iwe vipi hatocheza mpaka ruhusa rasmi ya klabu yake, labda tu awe hajaingia mkataba.

Ndicho kilichotokea, klabu hiyo imekiri kwamba haikuambiwa ukweli kuhusiana na mchezaji hali iliyosababisha wao kufanya makosa ya kuwasiliana na kumtumia mwaliko mchezaji mwenye mkataba unaozidi miezi sita bila kwanza kuwasiliana na klabu na kupata ruhusa ya kukubaliwa mwaliko huo. Klabu imekiri kukiuka taratibu na Kanuni za FIFA na imeona hatari iliyopo mbele yao.

Habari zinasema Simba iko tayari kumuachia Kibu aondoke, ila inataka kipengele ilichokiweka cha kuuzwa mchezaji huyo kifikiwe, ambacho ni dola za Kimarekani milioni moja, sawa na kiasi cha Sh. bilioni 2.7 za Kitanzania, wakiwa hawataki kusikia kuhusu majaribio kwa kuwa kuna kukosa na kupata, ikitokea akakosa na kurudi itakuwa imetoa mwanya kwa wachezaji wao wengine kuondoka kihuni.

Ina maana hapa Kibu amekwama. Kama ni akili yake mwenyewe au kuna waliokuwa wanamshawishi, basi hawakumshauri vizuri. Hatogusa mpira mpaka Simba waruhusu. Hili nadhani litakuwa fundisho kwa wachezaji wengine hasa wa Kitanzania.

Huku ndiko tunaona hata usajili wa timu mbili, huwezi kuona mchezaji yeyote wa kigeni kutoka nje kasaini timu mbili, utata kwenye usajili wake, au asajili timu halafu haendi kuitumikia, au anatimka nje.

Hili limefanywa pia na Lameck Lawi ambaye amechukua pesa za Simba, lakini kwa sasa ametimkia Ubelgiji. Kwa sasa Simba na Coastal ambazo ziliwashiana moto kuhusu suala hili, wameamua kukaa ili kulizungumza kama walivyoamriwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

Nadhani tabia hii imewafanya wachezaji wa Kibongo wasiaminike, na hii itawaponza zaidi huko mbele ya safari kwani klabu zitakuwa zikiogopa kuwasajili, badala yake kwenda nje kusajili wachezaji ambao wanafahamu maana ya mikataba na kuiheshimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live