Kocha wa Simba, Oliviera Robertinho amesema moja ya silaha muhimu alizonazo kwenye kikosi chake ni Kibu Denis ambapo anaweza kumbadilisha kumpa jukumu lolote gumu na akalitekeleza.
Kibu ambaye amekuwa na rekodi nzuri tangu msimu kuanza amecheza mechi muhimu zote za Simba zile za kimataifa na Ligi Kuu Bara na kufanya mambo makubwa.
Kibu ndiye aliyeifungia Simba bao la kwanza mchezo wa kwanza wa African Football League dhidi ya Al Ahly, mchezo ambao Simba walitoka sare ya 2-2.
Robertinho alisema anakoshwa na uwajibikaji wake ambapo amemshangaa kumtumia kama mshambuliaji wa kati na hesabu za kuufanya mfumo wa 4-3-3 walioutumia unakamilika vizuri na bado akafanikiwa kufunga bao muhimu.
Alisema anatamani wachezaji wake wengine wa eneo la ushambuliaji wangekuwa na nidhamu ya kucheza kwa maeneo kama ambavyo Kibu na nahodha wake John Bocco wanafanya.
“Watu wanaweza kuona sasa kwanini sisi makocha tunahitaji sana kumuona Kibu uwanjani na sio kukaa nje, ni mchezaji ambaye ukimpa majukumu ya kucheza kwa nidhamu ya nafasi ataifanya kwa kiwango kikubwa, nafahamu zipo changamoto za kiufundi kwake lakini anachokifanya ni kikubwa kuliko hizo changamoto.
“Ilikuwa uamuzi mgumu kuamua kumfanya kucheza kama mshambuliaji wa kati tena dhidi ya timu kubwa kama Al Ahly, lakini hata kama alifunga bao moja alifanya kila kitu kwa ubora mkubwa, tunahitaji wengine kucheza kama hivi, tuna Bocco pia anaweza kufanya hivi.
“Simba ni timu kubwa ina inatakiwa kuwa na mastaa wakubwa kama Kibu alivyo kwa sasa, lakini pia wawe wanaweza kubadilika badilika ili timu iwe na uhakika wa kumtumia muda wowote,” alimalizia Kibu.