Yanga inajiandaa kuanza maisha mapya bila ya kocha Nasreddine Nabi aliyekaushia mkataba mpya, huku akiwa ameweka heshima kubwa kwa miaka miwili na ushei akiwapa jeuri mashabiki wa klabu hiyo kutamba, lakini pale Msimbazi, kuna mtu kakaa miezi sita ila balaa lake sio mchezo.
Huyo sio mwingine ila ni kocha Robert Olivieira 'Robertinho', ambaye tangu aingie Simba Januari 3, 2023 kazi yake imemweka katika ramani kubwa ya heshima kwa kupiga kazi kubwa akiibeba timu hiyo kwa namba za hatari bila kujali nafasi ya pili iliyomaliza kikosi hicho nyuma ya Yanga.
HAJAPOTEZA MECHI BARA
Tuchukue mechi 11 ambazo Robertinho aliiongoza Simba katika duru la wa pili kuanzia ile ya Mbeya City jamaa hajapoteza mchezo wowote akitoa sare mbili pekee dhidi ya Azam FC na Namungo zote zikimalizika kwa timu zote kufungana bao 1-1.
Robertinho katika mechi hizo mbili aliangusha alama 4 huku akishinda mechi zingine 9 zilizosalia za ligi na kubaki kuwa mshindani mzuri mbele ya Yanga katika mbio za ubingwa, hadi dakika za lala salama watani wao wakatangaza ubingwa kabla ya mechi mbili kutokana na presha za Mbrazili huyo.
KASHINDA TISA
Robertinho akiwa Simba amefanikiwa kuiongoza timu hiyo kushinda jumla ya michezo 9 huku akitoa sare michezo miwili na kukusanya jumla ya alama 29 akiwazidi Yanga ambao katika michezo 11 walikusanya alama 28 wakizidiwa alama moja na wekundu hao.
Robertinho aliikuta Simba ikiwa nafasi ya pili na alama 44 huku Yanga ikiwa na alama 50 ambapo alama 29 zilimfanya kumaliza ligi na jumla ya alama 73 akizidiwa alama 5 na mabingwa Yanga ambao walimaliza na alama 78.
KAVUTA TATU KWA NABI
Kama kocha wa Yanga Nabi ataondoka basi kitu pekee atakachomtambia mwenzake ni mataji na kuifikisha timu yake Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini Robertinho alifanikiwa kuvuna alama tatu kwa mwenzake baada ya kumchapa kibabe kwa mabao 2-0 walipokutana kwenye ligi.
SIMBA INAFUNGA TU
Chini ya Robertinho Simba ilikuwa moto zaidi kwa kufunga mabao ambapo aliikuta ikiwa na mabao 47 huku watani wao Yanga wakiwa na mabao 37 lakini mpaka ligi inamalizika wekundu hao walimaliza kinara wa mabao wakifunga jumla ya mabao 75 huku bingwa akimaliza na mabao 61 ya kufunga.
HAT TRICK MBILI
Simba ilitengeneza Hat trick mbili chini ya Robertinho kupitia Jean Baleke na Saido Ntibazonkiza 'Saido' aliyemaliza ligi akiwa na jumla ya hat trick mbili akitangulia kuwa na moja wakati kikosi hicho kikiwa chini ya kocha wa muda Juma Mgunda.
Hadi ligi inamalizika Simba wakawa na jumla ya hat trick tano pamoja na zile mbili za nahodha John Bocco ambaye ndiye aliyetangulia kuwa na hat trick msimu huu uliomalizika huku watani wao Yanga wakiwa na hat trick mbili kupitia washambuliaji Fiston Mayele na Stephane Aziz KI.
NI SAIDO NA BALEKE
Staa wa Robertinho katika ufungaji ni Saido ambaye alifunga jumla ya mabao 10 chini ya kocha huyo akifuatiwa na Baleke aliyefunga 8, nyuma yao akiwa winga Pape Sakho aliyefunga mabao 4, huku beki Hennock Inonga, Israel Mwenda, Kibu Denis, Bocco na kiungo Clatous Chama kila mmoja akifunga bao moja na kufanya jumla wote kufunga mabao 27 ambapo Azam wakimzawadia bao moja la kujifunga kupitia beki Abdallah Kheri aliyejifunga wakati timu hizo zilipokutana.
Saido pia alionyesha umwamba zaidi kwa kuingia kwenye rekodi ya kuwa nyota wa kwanza wa kigeni nchini kufunga mabao mabao kwenye mchezo mmoja, akifuata nyayo za Nsa Job aliyefunga 2009 wakati akiwa na Azam ilipoilaza Villa Squad kwa mabao 6-2 na kuwa nyuma ya Edibily Lunyamila aliyeshikilia rekodi ya kufunga mabao sita kwenye mechi moja walipoizamisha Kagera Stars kwa mabao 8-0 msimu wa 1998.
VIPIGO VIKALI
Ushindi mkubwa kwa robertinho kwenye ligi ni pale alipowatandika Polisi Tanzania kwa mabao 6-1 ndani yake akizalisha hat trick ya Saido, lakini kwenye Ligi ya Mabingwa alifanya kufuru kwa kuinyoa Horoya AC ya Guinea kwa mabao 7-0 katika mechi ya hatua ya makundi.
Pia chini ya Robertinho, hakuna mechi yoyote ambayo Simba ilicheza kwenye ligi au katika michuano ya ASFC bila kufunga bao, kuonyesha mbinu zake za kusaka mabao ni kubwa na wachezaji alionao hawajawahi kumuangusha, licha ya kwenye mechi za kimataifa alicheza mechi kadhaa bila kufunga.
AKWAMA HUKU
Robertinho mtihani pekee ambao atabaki nao ni kimataifa ambapo alishindwa kuifanya Simba kuvuka hatua ya robo fainali kama ambavyo watangulizi wake walivyoshindwa ambapo alijikuta safari yake ikihitimishwa na kaimu bingwa wa msimu huu Wydad kwa penalti 4-3 ugenini baada ya timu zote kushinda kwa bao 1-0 kila mmoja ilipokuwa nyumbani.
Kabla ya hatua hiyo Robertinho alimaliza nafasi ya pili katika makundi baada ya kushinda mechi 3, akipoteza pia 3 na kuifanya Simba kumaliza makundi wakiwa na jumla ya alama 9 kwewnye kundi ambalo liliongozwa na Raja Athletic ya Morocco ambao waliwachapa wekundu hao nyumbani na ugenini wakiungana na Horoya ambao walikuwa wa kwanza kuichapa Simba kwenye mchezo wa kwanza.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumzia kiwango hicho Robertinho alisema ubora huo ambao timu yake iliuonyesha katika mechi hizo 19 za kimashindano kwenye mechi za ligi ya ndani na ligi ya mabingwa ulitokana wachezaji wake kushika haraka falsafa ya soka lake.
Hata hivyo Robertinho alisema bado Simba inatakiwa kuonyesha ubora mkubwa zaidi ya huo na kurudi kusaka mataji kwa msimu ujao endapo utafanyika usajili mkubwa kwa kikosi chake.
"Ndani ya muda mfupi kitu ambacho kilinifurahisha ni jinsi wachezaji walivyoingia katika mfumo wangu, tulikuwa tunacheza soka la kushambulia tunapokuwa na mpira lakini pia tunazuia kwa pamoja tunapokosa mpira, hii iliwafanya wachezaji wote kufanya kazi kama familia,"alisema Robertinho ambaye yuko kwao Brazil kwa mapumziko.
"Tunatakiwa kurudi na gia kubwa kwa msimu ujao, Simba ni timu kubwa inatakiwa kurejea kwenye ramani ya kuchukua mataji, kama utafanyika usajili mkubwa kama ambavyo tumepanga na uongozi naamini msimu ujao tutakuja tofauti zaidi.