Anaandika mchambuzi nguli, Shaffih Dauda;
"Niliposema watu/kampuni nyingi zinatamani Simba imalize nafasi ya pili juu ya Azam FC ili ishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, sikuwa najizungumzia mimi kwamba ndio mnufaika pekee kibiashara bali kuna watu/kampuni/taasisi nyingi zitanufaika na Simba kwa sababu ya fan base yake kuliko Azam FC.
"Ukifanya utafiti mdogo kwenye hizi kampuni za TV [Azam TV, DStv, StarTimes] ambazo zinanunua haki za matangazo kuonesha mashindano ya Afrika, ukiuliza kati ya Simba na Azam wangetamani timu gani imalize Ligi katika nafasi ya pili hakuna hata kampuni moja ya TV itakwambia Azam FC!
"Kwa nini? Kwa sababu Azam ikimaliza nafasi ya pili na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ni watu wangapi watalipia ving’amuzi vyao kutazama mechi ya Azam FC vs Petro de Luanda? Lakini vipi kwa Simba?
"Kwa sababu hizohizo za kibiashara, hata Azam TV wanatamani sana Simba imalize Ligi ikiwa nafasi ya pili juu ya Azam FC kwa sababu wanajua itawalipa kwenye biashara yao na watapiga mpunga zaidi kupitia subscriptions ya ving’amuzi kuliko timu yao ikifuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Bila shaka hata Simba ilipoifunga Azam FC [Azam 0-3 Simba], watu wa Azam TV walifurahi sana wakijua mbio za kuwania nafasi ya pili zimekwisha! Wakiamini biashara yao itachangamka ikifika msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Ni kitu kizuri na kikubwa kwa Azam FC kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu ya kujitambulisha na kuweka alama kwenye soka la Afrika kama klabu lakini kibiashara hawauzi sokoni ukilinganisha na Simba."