Ingizo jipya ndani ya Klabu ya Yanga, Nickson Kibabage amesema yuko tayari kwa ajili ya changamoto mpya za msimu wa 2023/24.
Kibabage amejiunga na Yanga kwenye dirisha hili kubwa la usajili akitokea Singida Fountain Gate.
Akizungumza na Yanga Media, Kibabage amesema anajua changamoto kubwa inayomkabili mbele lakini yeye yuko tayari kupambana kuhakikisha anaisaidia Yanga.
“Najua nimekuja katika Klabu kubwa zaidi, ushindani wa namba hapa ni mkubwa zaidi. Kuna mkusanyiko wa wachezaji wengi wakubwa hapa, hivyo ni jukumu letu wachezaji kupambana kuleta matokeo mazuri,” alisema Kibabage.
Kibabage amekuwa mchezaji wa kwanza wa Yanga kutambulishwa kwenye dirisha hili la usajili na alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichosafiri kwenda Malawi kushiriki mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Nyassa Big Bullets.