Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Khalid Aucho na hadithi ya Jasho na kilio cha Samaki

Khalid Auchoooooooo Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwenye kitabu kitakatifu chenye orodha ya wachezaji muhimu wanaobeba ramani ya vita pale Jangwani hauwezi kushangaa kuliona jina la khalid Aucho likichomoza kwenye orodha ya tatu bora.

Ni Aucho ndiye anaamua timu icheze mdundo gani kwa wakati gani. Akitaka icheze sebene au mchiriku timu itacheza hivyo jinsi anavyotaka yeye.

Furaha ya Jux kwenye biti za Maneke, huenda si chochote pindi Miguel Gamondi akipata fursa ya kuanza na Aucho kwenye kikosi chake, furaha ilioje kuwa na mbeba ramani wa vita mtiifu.

Kwenye kurasa za vitabu vya soka huenda jina la Khalid Aucho limeandikwa kwa penceli isiyokolezwa vyema, ni muendeleo wa vita kati ya dunia na viungo wakabaji. Utaliandika vipi jina lake kwa peni iliyokolezwa vyema wakati hauwezi kumkuta akiassist wala akifunga mara kwa mara.

Jina la Pacome litaimbwa na kupigwa muhuri kwenye kila kurasa za vitabu vya soka sababu ya assist zake na magoli yake yanayoacha kumbukumbu njema kwenye mifumo ya ubongo ya kila shabiki.

Khalid Aucho na jasho lake ni muendelezo wa hadithi ya kilio cha samaki ambacho kilio chake hakitambuliki wala kuonekana na walimwengu.

"Ninafikiri ni mchezaji muhimu zaidi kiwanjani hasa ninapoamua staili yetu ya kucheza, jipe muda kumtazama yeye badala ya mpira ili unielewe, vinginevyo utaniletea idadi ya assist hapa" ni maneno ya kocha wa hispania akimzungumzia Sergio Busquets kwenye kikosi chake. Hispania ile iliyochukua kombe la dunia pamoja na Euro 2012.

Maneno ya kocha wa hispania yalibeba ujumbe tosha akiwa anatukumbusha kuipa heshima miguu ya Segio Busquets na viungo wanaocheza eneo hilo.

Khalid Aucho si muhanga wa kwanza na hatokuwa wa mwisho juu ya laana ile ya kutotambulika kwa jasho lao. Huenda hakuna anayelitolea macho sana jasho lake sababu jasho lake hutumika sehemu isiyofaa machoni mwa watu wengi.

Khalid Aucho ni miongoni mwa wabeba ramani ambao jasho lake linakwenda zake kama kilio cha samaki majini

Chanzo: www.tanzaniaweb.live