Staa, Kevin De Bruyne ameanza kuzua hofu huko Manchester City baada ya kukiri kwamba anashawishika na mpango wa kwenda Saudi Arabia.
Kiungo huyo mchezeshaji wa Ubelgiji amekuwa mchezaji muhimu huko Man City tangu alipotua kwa uhamisho wa pesa nyingi kutoka Wolfsburg.
Aliiwezesha Man City kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, ukiwa ni ubingwa wao wa nne mfululizo kwenye ligi hiyo.
Akibakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, alisema kwamba anafikiria mpango wa kuhamia Saudi Arabia.
De Bruyne alisema: “Kama umri wangu nimefungua milango kwa kila kitu. Unazungumzia ishu ya kiwango cha pesa na namna ya kumaliza maisha ya soka. Wakati mwingine unaweza kufikiria juu ya hilo. Kama nitacheza huko (Saudi Arabia) kwa miaka miwili, nitaweza kuvuna pesa nyingi sana.”
De Bruyne alicheza kwa kiwango bora msimu uliopita, akifunga mabao sita na kuasisti mara 18 kwenye michuano yote, licha ya kukosa sehemu kubwa ya msimu huo kutokana na kuwa majeruhi.
Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea anafikiria kuhusu maisha yake ya baadaye. Klabu kadhaa za Saudi Arabia zimekuwa zikizungumza na wawakilishi wa mchezaji huyo zikipiga hesabu za kumsajili, huku miamba ya Ligi Kuu Marekani, San Diego FC nayo inahitaji huduma yake.
“Bado nina mkataba wa mwaka mmoja umebaki, hivyo lazima nianze kufikiria nini kitatokea. Mwanangu wa kwanza ana miaka minane na anachokiuliza yeye ni kucheza soka England, anauliza nitacheza Man City kwa muda gani. Hivyo, ni lazima kuanza kufikiria hilo.”€
Mastaa kibao wa zamani wa Man City, akiwamo Riyad Mahrez na Aymeric Laporte walihamia Saudi Arabia wakati wa majira ya kiangazi yaliyopita kwenda kupiga soka na pesa.