Benjami Mendy amejikuta kwenye mapambano mazito ya kusafisha jina lake kiasi cha kusababisha auze mali zake, magari na saa za kifahari na kupata hasara zaidi ya Pauni 1 milioni (Sh 3.2 Bilioni)
Staa huyo wa zamani wa Manchester City, alikutwa hana hatia kwenye kesi ya kubaka iliyokuwa ikimkabili, lakini wakati hukumu hiyo inatolewa tayari beki huyo wa kushoto amepoteza mali zake nyingi.
Mendy tayari alikuwa milionea wakati anajiunga na Man City akitokea Monaco 2017 na kusaini mkataba wa miaka sita, ambapo alikuwa akilipwa mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki na bonasi iliyokuwa ujira wake wa wiki uliokuwa unafika Pauni 170,000. Lakini, badala ya kuvuna Pauni 31.2 milioni kwenye dili lake hilo, amejikuta akipambana asiwe mfilisi baada ya mwaka 2020 ambao alikamatwa kwa madai ya kubaka.
Alilazimika kufunga kampuni yake ya haki zake za taswira baada ya kusumbuliwa na mamlaka za kodi. Mendy alijikuta kwenye tatizo kubwa la kiuchumi baada ya kufunguliwa mashtaka ambapo Man City ilisitisha kumlipa mishahara mara moja baada ya kesi kufunguliwa.
Kwa kipindi hicho tayari alikuwa amelipwa Pauni 5 milioni, lakini kwa kuwa alikuwa na maisha na staili yake ya kupiga bata kabla ya kukumbwa na janga hilo, hakuwa na mashaka yoyote kama ingefika siku angepatwa na jambo. Matokeo yake akalazimika kulipiga bei jumba lake la vyumba sita lililopo kwenye eneo maarufu la The Spinney, Prestbury, Cheshire, aliuza pia gari zake za kifahari ikiwamo Lamborghini na saa za bei mbaya.