Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kenya, Zimbabwe wafungiwa kujihusisha na soka

Fifa Kenya, Zimbabwe wafungiwa kujihusisha na soka

Thu, 24 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirikisho la kandanda duniani, Fifa, Alhamisi limeipiga marufuku Kenya na Zimbabwe kushiriki katika shughuli zote za kandanda kutokana na hatua ya serikali kuingilia masuala yake.

Rais wa Fifa Gianni Infantino amethibitisha kusimamishwa kwa muda kwa shughuli zote za soka wakati wa mkutano na wanahabari wa baraza la Fifa.

"Bila ya kuathiri uchunguzi wowote wa mamlaka ya kitaifa au vyombo vingine vya mahakama, baraza la Fifa pia liliamua kusimamisha Shirikisho la Soka la Kenya na Chama cha Soka cha Zimbabwe mara moja kutokana na kuingiliwa isivyofaa na serikali ," Infantino alisema.

Waziri wa michezo nchini Kenya Amina Mohammed , tarehe 11 Novemba mwaka uliopita alilifutilia mbali shirikisho la soka nchini Kenya FKF lililokuwa likiongozwa na Nick Mwendwa na badala yake kuunda kamati simamizi, miongoni mwa masuala mingine , ili kuendesha soka kulingana na katiba ya shirikisho hilo.

Katibu mkuu wa Fifa fatma Samoura, aliandikia serikali ya Kenya mara mbili baada ya kuvunjwa kwa shirikisho la FKF , akiitaka serikali , kuirudisha ofisini kamati ya shirikisho hilo ili kuendelea kutafuta suluhu.

Rais wa shirikisho la soka FKF nchini Kenya Nick Mwendwa alikamatwa katika matukio mawili tofauti na kushtakiwa kwa kushiriki katika ufisadi kabla ya kujiuzulu.

Lakini hatua hiyo ya kuivunjilia mbali FKF ilitajwa kuwa haramu na Fifa huku ikitoa vitisho vya kupiga marufuku soka nchini. Shirikisho hilo katika msururu wa mawasiliano yake na serikali lilisisitiza kurudishwa ofisini kwa FKF na kuanzisha mipango ya majadiliano ili kutatua tatizo lililopo.

Je marufuku hiyo ina maana gani?

Kusimamishwa kwa Kenya kunamaanisha kuwa nchi hiyo itazuiwa kushirikisha timu yoyote katika mashindano yoyote nje ya kimataifa. Hizi ni pamoja na timu za wanaume na wanawake na vilabu.

Vile vile, marefa watazuiwa kushiriki katika majukumu ya kimataifa ilhali hakuna mchezaji wa Kenya anayeishi humu nchini atakayeruhusiwa kukamilisha uhamisho wa kikazi katika muda huo.

Licha ya waziri Amina kuwahakikishia Wakenya mara kadhaa kuwa serikali inawasiliana na Fifa na kudhibiti shughuli zote za kandanda, timu ya taifa ya soka ya wanawake Harambee Starlets ilizuiwa kushiriki katika awamu ya mwisho ya mchujo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika miongoni mwa Wanawake dhidi ya Uganda.

Kulingana na gazeti la Nation nchini Kenya, mnamo Januari 28 mwezi uliopita, CAF ililiandikia shirikisho la soka la Uganda, Fufa, kulifahamisha kwamba timu yao imefuzu kwa michuano ya kandanda ya bara baada ya Kenya "kujiondoa kwenye mashindano."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live