Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ken Gold yakiri kuzidiwa ujanja

Ken Gold Kileleni Ken Gold yakiri kuzidiwa ujanja

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kutibuliwa mipango na Pamba Jiji, Kocha Mkuu wa Ken Gold ya Mbeya, Jumanne Charles, amesema wapinzani wao waliwazidi mbinu na ufundi uwanjani huku akitamba kuwa kazi ya kuisaka nafasi ya kwenda Ligi Kuu haijaisha kwani mipango sasa inahamia kwenye mechi zijazo.

Timu hiyo ambayo ilikuwa kileleni mwa Ligi ya Championship, Jumapili ilichapwa ugenini mabao 2-1 mbele ya Pamba Jiji katika Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa hivyo kutibua mipango na matumaini yake ya kuendelea kuongoza ligi hiyo.

Kichapo hicho ni cha pili msimu huu kwa matajiri hao wa Dhahabu kutoka Chunya, kipigo cha kwanza walikipita Oktoba 1, 2023 ugenini dhidi ya Mbeya Kwanza wakifungwa bao 1-0.

Mabao ya Pamba Jiji yalifungwa na Mudathir Said pamoja na Aniceth Revocatus ambao wamefikisha mabao matatu kila mmoja na kuwa vinara katika timu hiyo huku William Edgar wa Ken Gold akiongoza kwa mabao nane.

Akizungumza baada ya kipigo cha Pamba, Charles alisema kikosi chake kilicheza vibaya kikishindwa kutengeneza nafasi nzuri za kufunga na kufanya makosa ambayo wapinzani wao waliyatumia vyema na kupata mabao.

Alisema walijua tangu mwanzo mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa Pamba walikuwa wametoka kupoteza mechi iliyopita hivyo walihitaji ushindi wa lazima, ambapo benchi lake liliandaa mpango mzuri wa mechi hiyo lakini walifeli kiufundi kuufanyia kazi uwanjani ndani ya dakika 90.

“Tulijua Pamba walipoteza mchezo uliopita kwahiyo waliutaka ushindi tumejaribu kupambana nao lakini wametuzidi, tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi kufanyia kazi tunaamini tutarudi vizuri na kuanza kupata tena ushindi,” alisema Charles

Wakati huo huo, kocha mkuu wa Pamba Jiji, Mbwana Makatta alisema wachezaji wake kwa sasa wamepevuka na kuacha kufanya makosa ya kujirudia yasiyo ya lazima huku wakitumia vyema na kwa usahihi nafasi za mabao zinazotengenezwa.

“Malengo yamefikiwa na kupata pointi tatu nashukuru vijana sasa wamepevuka hawafanyi tena makosa mengi wamejirekebisha tofauti na huko mwanzo hata zile nafasi chache tunazopata tunazitumia,” alisema Makatta

Kwa ushindi huo Pamba imeendelea kuweka matumaini yake ya kupanda daraja kuwa hai ambapo imepanda kutoka nafasi ya tano hadi ya nne ikifikisha pointi 21, huku Ken Gold na Mbeya Kwanza ambazo zilipoteza mechi zao za mwishoni mwa wiki zikiwa na alama 23 kila mmoja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: