Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ken Gold yaishusha kileleni Mbeya Kwanza

Ken Gold Kileleni Ken Gold yaishusha kileleni Mbeya Kwanza

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Ken Gold imefanikiwa kuongoza msimamo wa Ligi ya Championship baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 mbele ya Copco FC ya Mwanza, huku nyota wake, William Edgar akiendelea kung’ara kwenye upachikaji mabao.

Ken Gold ya mkoani Mbeya imepata ushindi huo ugenini jana Novemba 12, 2023 kwenye mchezo huo wa mzunguko wa 10 ambao umechezwa katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.

Baada ya ushindi huo, timu hiyo inafikisha pointi 23 sawa na Mbeya Kwanza, lakini faida ya mabao mengi ya kufunga 18 na ya kufungwa manne yameipeleka kileleni, huku Mbeya kwanza ikiwa imefunga mabao 15 na kuruhusu sita.

Katika mchezo huo ambao umechezeshwa na mwamuzi, Japhet Smati kutoka Katavi ambayo amekuwa akipigiwa kelele na kuzomewa na mashabiki ambao hawakuridhishwa na maamuzi yake, zimepatikana penalti mbili akiwazawadia Ken Gold dakika ya sita na Copco dakika ya 52.

Wageni, Ken Gold ndiye wamekuwa wa kwanza kupata bao dakika ya sita kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Robert Makidala lakini Copco wakasawazisha bao hilo dakika ya 19 kupitia kwa Abdulkarim Segeja.

Ken Gold wamepata bao la pili dakika ya 22 likifungwa na mshambuliaji wao kinara, William Edgar hata hivyo, Copco wakasawazisha dakika ya 52 kwa mkwaju wa penalti ukifungwa na Abdulkarim Segeja.

Wakati wenyeji Copco wakiwa na matumaini ya kuondoka na pointi moja mbele ya timu hiyo ngumu, matumaini yao yameyeyuka baada ya William Edgar kuifungia Ken Gold bao la tatu dakika ya 79 na kuipeleka timu yake kileleni.

Mabao mawili ambayo wamefunga, Abdulkarim Segeja (Copco) na William Edgar (Ken Gold) yamewafanya wafikishe mabao saba kila mmoja katika mechi 10 za ligi hiyo wakiendelea kuchuana kwenye vita ya ufungaji mabao, wakifuatiwa na Salim Aiyee wa Mbuni (6).

Kocha wa Ken Gold, Jumanne Challe, amesema matokeo hayo yametokana na mpango mzuri wa mechi ambao aliuandaa kwa kuwafahamu Copco ambao ni wazuri kwenye kumiliki mpira na kupiga pasi fupi, hivyo, ameamua kutumia mipira mirefu na imewalipa.

Chanzo: Mwanaspoti