Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ken Gold, Mbeya Kwanza ngoma ngumu

Ken Golddddddd Ken Gold, Mbeya Kwanza ngoma ngumu

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kutesa katika mechi zilizopita, Ken Gold imepunguzwa kasi kwa kuambulia suluhu ya bila kufungana dhidi ya Mbeya Kwanza katika mchezo wa Ligi ya Championship.

Mchezo huo ambao umepigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, licha ya kila timu kuhitaji ushindi, lakini hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyoliona lango la mwenzake.

Hata hivyo, pamoja na juhudi binafsi za mchezaji mmoja mmoja kwa kila timu, lakini hali ya uwanja haikuwa rafiki kutokana na nvua iliyobyesha na kusababisha mwamuzi wa mechi hiyo kusimamisha mchezo kwa dakika kadhaa.

Mchezo huo ulikuwa wa kisasi na rekodi kufuatia mzunguko wa kwanza Ken Gold kufungwa bao 1-0, hivyo kutaka kulipa kisasi huku wapinzani wake wakihitaji kuendeleza ushindi na mipango kuwa migumu.

Pamoja na matokeo hayo, Ken Gold inabaki kuongoza msimamo kwa pointi 43 huku Mbeya Kwanza ikibaki katika nafasi ya tano ikiwa na alama 36 baada ya timu zote kucheza michezo 19.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Ken Gold, Jumanne Challe amesema pamoja na kushindwa kubakiza alama tatu, lakini pointi moja si haba kwani inawabakiza kileleni.

"Mbinu za ufundi zilishindwa kutumika kutokana na hali ya uwanja zikabaki juhudi za mchezaji na maelekezo kadhaa ya benchi (la ufundi), lakini bado tunabaki juu," amesema kocha huyo.

Kocha mkuu wa Mbeya Kwanza, Michael Mnyali amesema walipania kushinda mchezo huo kutokana na mechi iliyopita kupoteza dhidi ya Mbeya City, lakini mvua iliharibu mipango yao.

"Zile pasi za chini chini zilipotea kwa sababu utulivu ulikosekana uwanjani, mvua iliharibu kila kitu ila tunaenda kujipanga tena na mechi zinazofuata," amesema Mnyali.

Chanzo: Mwanaspoti